Marekani yaeleza wasiwasi wake kwa kukamatwa viongozi wa upinzani Tanzania

Mwakilishi Karen Bass, Mdemokrat, kutoka California

Kamati ya Wabunge wa Marekani imeelezea wasiwasi wake juu ya kukamatwa kwa kiongozi wa upinzani nchini Tanzania, Freeman Mbowe, na maafisa wengine kumi na moja.

Taarifa iliyotolewa na Karen Bass, Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya mambo ya nje, kuhusu bara la Afrika, imesema kuwa: "Kifo ambacho hakikutarajiwa cha Rais wa Tanzania, John Magufuli, kilikuwa mshtuko wa kweli kwa wote.

Lakini uteuzi wa Makamu wake wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ulionekana kama wa kuisogeza mbele nchi hiyo kwenye njia ya kidemokrasia zaidi.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania

Taarifa hiyo inaongeza kwamba kwa bahati mbaya kukamatwa kwa Mbowe na viongozi wengine wa upinzani kumepunguza matumaini hayo.

Polisi wa Tanzania Alhamisi walisema Mbowe aliyekamatwa juzi Jumatano, atakabiliwa na mashtaka kadhaa, yakiwa ni pamoja na kupanga njama za kufanya vitendo vya kigaidi na kuua maafisa wa serikali.

Mwanasiasa huyo amekanusha mashtaka hayo na chama chake cha Chadema kilimnukuu akisema kwamba yuko tayari kwa kesi hiyo, aliyoiita “ya uzushi.”

Hadi tukitayarisha ripoti hii, Mbowe na watuhumiwa wenzake hawakuwa wamefikishwa mahakamani, huku polisi wakisema kwamba wanawashikilia kwa mahojiano zaidi.

Kukamatwa kwao mjini Mwanza kumevutia ukosoaji mkubwa, kutoka pande mbalimbali ikiwemo mashirika ya haki za binadamu, na vyama vingine vya upinzani nchini humo.

Chanzo cha habari : VOA News