Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 05:36

Mwanasiasa wa Tanzania Godbless Lema akimbilia Kenya, akamatwa Pamoja na familia


Godbless Lema aliyekuwa mbunge wa Arusha akizungumza bungeni (Picha ya Maktaba)
Godbless Lema aliyekuwa mbunge wa Arusha akizungumza bungeni (Picha ya Maktaba)

Msako dhidi ya wanasiasa wa upinzani unaendelea nchini Tanzania, siku chache baada ya rais John Magufuli kuapishwa kwa muhula wa pili madarakani.

Aliyekuwa mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema, ambaye alishindwa katika uchaguzi wa mwezi uliopita baada ya kuhudumu kwa mihula miwili bungeni amekamatwa na anazuiliwa katika kaunti ya Kajiado nchini Kenya baada yake na familia kutoroka Tanzania na kuingia Kenya.

Kulingana na wakili wa Lema George Luchiri Wajackoyah, polisi wamemkamata pamoja na familia yake. Wakili Wajackoyah naye alikamatwa kwa muda.

Namna alivyovuka mpaka wa Tanzania na Kenya

Vyanzo vya habari vimesema kwamba mkewe Lema na familia yake, walikuwaa wamekataliwa kuvuka mpaka na maafisa wa uhamiaji wa Tanzania kwenye mpaka wa Namanga wakitaka aambatane na mume wake.

Baadaye alitoa sababu kwamba anakwenda kuwatafutia watoto wake shule nchini Kenya, ndipo akaruhusiwa.

Vyanzo hivyo vinaeleza kwamba Lema alivuka mpaka baada ya kuwaambia maafisa wa uhamiaji kwamba alikuwa anaenda kubadilisha pesa ili afanikishe shughuli ya mkewe.

Alipovuka mpaka, aliondoka kwa gari binafsi, na maafisa wa polisi Tanzania walipogundua kwamba amewakwepa, waliwapigia simu maafisa wa Kenya na kuripoti kwamba kuna mtu ameingia nchini Kenya kutoka Tanzania bila idhini, na kwamba lazima akamatwe na kurudishwa Tanzania.

Katika mahojiano ya simu na Sauti ya Amerika, wakili wa Godbless Lema amesema kwamba alifika mpakani Jumapili asubuhi kumsaidia mteja wake.

“Nimepigiwa simu na mheshimiwa Godbless maanake mimi ni wakili wa chama cha Chadema, wakili wake, wakili wa Mbowe na wakili wa Tundu Lissu. Alinipigia simu akaniambia Prof, njoo Namanga nataka kukuona. Nimemkuta na mama na watoto watatu. Ameniambia anakambia Tanzania kutokana na hali ya siasa ilivyo. Kwamba amechoka kushikwa na heri auwawe akiwa Kenya kuliko akiwa Tanzania.” Amesema Wakili George Luchiri Wajackoyah akiongezea kwamba wamekamatwa wakiwa safariki kuelekea ofisi za umoja wa mataifa za kuwahudumia wakimbizi UNHCR.

Alivyokamatwa na polisi wa Kenya

“Tumevamiwa na maaskari karibu 20, tukashikwa na kupelekwa wote kwenye kituo cha polisi cha Ilbisil. Nimewaambia polisi kwamba Godbless na familia yake ni wahamiaji wanatafuta hifadhi.” Ameendelea kusema George Luchiri Wajackoyah katika mahojiano na idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika akiongezea kwamba walipowaeleza polisi kwamba yeye ni wakili na wenzake waliokamatwa nao walikuwa wanakimbia nchi yao, wakahamishiwa katika kituoc ha polisi cha Kajiado, ambapo Godbless anazuiliwa. Wakili George na familia ya Godbless, wameachiliwa huru.

Kulingana na wakili George, Godbless alikataa kutumia njia za kisheria kuvuka mpaka wa Tanzania na Kenya kwa kuhofia kwamba angekamatwa. Vile vile, alitumia gari la umma maarufu ‘dala dala’ kusafiri ili asitambuliwe kwa rahisi.

Sheria ya UNHCR kuhusu watu wanaokimbia nchi yao na kutafuta hifadhi nchi nyingine

Kabla ya uchaguzi mkuu, kulikuwa na madai ya wanasiasa wa upinzani kukamatwa na maafisa wa polisi na wengine kadhaa wamekamatwa baada ya uchaguzi huo.

“Godbless ameniambia ameshikwa mara 25 na amekuwa akipigwa kila mara anapigwa. Wakati nipo katika kituo cha polisi, nimekuwa nikisia mawasiliano kati ya polisi wa Kenya na Tanzania wakitaka Godbless arudishwe Tanzania haraka iwezekanavyo.” Akiongezea kwamba “kulingana na ibara ya 2 ya sheria za UNHCR za mwaka 1951 mtu yeyote anayekimbia nchi yake kwa kuhofia maisha yake, hastahili kuwa na stakabadhi za utambulisho ndio maana nimemwaacha mikononi mwa polisi kama mhamiaji anayetafuta hifadhi.”

“Nimeongea na ofisi ya UNHCR, Amnesty International na wahusika wengine wote. Nitashughulikia swala hili kikamilifu Jumatatu asubuhi”. Amesema wakili George.

Wanasiasa wa upinzani waendelea kukamatwa Tanzania, wengine waenda mafichoni

Mgombea wa urais katika uchaguzi wa mwezi uliopita Tundu Lissu, anaishi katika ubalozi wa ujerumani mjini Dar-es-salaam kwa kuhofia maisha yake.

Chama cha upinzani Tanzania – Chadema, kimekataa kutambua ushindi wa rais John Magufuli kikisisitiza kwamba uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba, ulikumbwa na wizi mkubwa wa kura.

Kiongozi wa chama hicho Freeman Mbowe anazuiliwa na polisi Tanzania, baada ya kukamatwa wiki iliyopita.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC.

XS
SM
MD
LG