Marekani : Baraza la Wawakilishi lakutana kupiga kura kumshtaki Rais Trump

Bunge la Marekani wakati taifa na dunia ikisubiri kura ya kumfungulia rasmi mashtaka Rais Donald Trump.

Baraza la Wawakilishi la Bunge la Marekani linakutana katika kikao cha kihistoria Jumatano kupiga kura kumfungulia rasmi mashtaka Rais Donald Trump.

Wakati wabunge wanakutana viongozi wa Baraza la Seneti hawajakubaliana jinsi kesi hiyo itakavyoendelea na ikiwa mashahidi wataruhusiwa katika kesi hiyo.

Wakati hayo yakiendelea maandamano ya kuunga mkono kesi hiyo kuendelea yamefanyika New York na miji mingine mikubwa ya Marekani, Jumanne usiku.

Wakati huohuo Kamati ya kanuni ya baraza la wawakilishi linaloshikiliwa na wademokrats lilikutana jana na kupitisha kanuni za jinsi upigaji kura wa kumfungulia mashtaka rais utakavyoendelea.

Wabunge watapigia kura shitaka la kwanza la utumiaji vibaya madaraka kwa kuitaka Ukraine kumchunguza mpinzani wake wa kisiasa Joe Biden. Na kupigia kura shitaka la pili la kuzuia hati na mashahidi wanaofahamu vyema kadhia hiyo kutoa ushahidi.

Warepublikan ambao wanamuunga mkono rais wanaendeelea kulalamika kwamba utaratibu wa kumshtaki ni wa uonevu.

Tome Cole mbunge wa chama cha Republican anasema Wademokrats hawajaweza kudhihirisha kwamba rais amefanya makosa.

Tome Cole amesema : "Kitu ambacho si fahamu ni kwanini waliowengi wanaendelea na utaratibu ambao unaegemea upande mmoja. Kwa nini wanaendelea, wakati wamarekani wengi hawako pamoja nao."

Ikulu kwa upande wake inajitayarisha kesi itakayoanza kusikilizwa mwezi Januari 2020, na rais Trump hapo jana alishambulia tena utaratibu mzimi wa mashtaka hayo.

Donald Trump alieleza: "Ni njama ya uwongo, uwonevu, ni kutafuta kisingizio. Hakuna kosa lililotendeka. Ninadhani hili ni jambo baya sana kwa kutumia chombo cha kumfungulia mashtaka rais ambacho ni adhimu, kutumiwa kwa ajili ya mawasiliano ya simu ya kawaida."

Rais Trump vile vile amempelekea Spika wa Bunge Nacy Pelosi barua ya kurasa 6 akieleza hasira zake na kukosoa vikali mashtaka wanaotaka kumfungulia.

Na katika upande wa pili wa bunge kwenye Baraza la Seneti maseneta wa chama cha rais cha republican wamesema watahakikisha kesi inafanyika kwa haraka kabisa.

Mkuu wa Seneti Mitch McConnell aliyekataa awali ombi la kiongozi wa walio wachache Mdemokrat Chuck Schumer la kutaka washauri wanne wa karibu wa rais kutoa ushahidi, anasemekana huenda akakubali jambo hilo kutendeka lakini kwa masharti watakayo kubaliana.

Mivutano na mashauriano hayo ya kisasa yakiendelea mamia ya wapinzani wa Trump waliandamana katika miji kadhaa mikubwa kutaka utaratibu kuendelea

Rodolph Pongon muandamanaji alieleza : "Baraza la wawakilishi limepanga kesi ya kuaminika inayo onyesha mabaya aliyofanya Rais. Na hivyo ninadhani ni muhimu sana hivi sasa kwa wapiga kura kulifahamisha bunge kwamba wanaunga mkono utaratibu wa kumfungulia mashtaka rais."

Hivi sasa nchi nzima inasubiri wabunge kumaliza mdahalo wa masaa sita Jumatano juu ya mashtaka hayo kabla ya kupiga kura.

Na wakimfungulia mashtaka, Trump atakuwa rais wa tatu wa Marekani kukabiliwa na hali hiyo baada ya Andrew Johnson na Bill Clinton.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.