Mapigano DRC yakosesha makazi watu zaidi ya 80,000

Jenerali Syvlvain Ekenge(VOA/ERikas Mwisi)

Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya watu 80,000 wamekoseshwa makazi kutokana na mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na wanauhitaji mkubwa wa chakula.

Mapigano baina ya wanajeshi wa serikali na waasi wa M23 yameongezeka katika jimbo la Kivu kaskazini.

Mapigano yalienea upande wa kusini mapema wiki hii kiasi cha kilomita 20 kutoka mji mkuu wa Goma, wa jimbo la Goma.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kibinadamu OCHA imesema wale waliokimbia makazi yao wamekwenda katika maeneo yaliyoboreshwa, ikiwemo Makanisa na shule.

Mashirika ya kibinadamu yanahofia kutokea hali mbaya kwa wakimbizi kama uhasama utaendelea.

Katika taarifa yake ya Jumatano msemaji wa Gavana katika jimbo hilo alisema wanakabiliwa na hali ya wasiwasi.

Hata hivyo Gavana wa kijeshi Jenerali Sylvain Ekenge katika jimbo la kivu kaskazini ametoa wito kwa watu kuwa watulivu na kutotumbukia katika hali ya taharuki.

Waasi wa M23 waliripotiwa kudhibiti maeneo takriban kilomita 25 kutoka mji wa Goma, ingawa Generali Ekenge alisema kuwa waasi walisukumwa nyuma.