Mapigano yameongezeka tangu jumatatu usiku, waasi wakidhibithi sehemu za mpakani karibu na Uganda a Rwanda.
Waasi wa M23 wanaripotiwa kuteka sehemu kadhaa zilizokuwa zinashikiliwa na wanajeshi wa serikali, ikiwemo kambi ya jeshi ya Kibumba, iliyo kilomita 15 kutoka mji wa Goma.
Waasi hao walishambulia wanajeshi wa serikali kuanzia Jumatatu na kusababisha raia wa DRC kukimbilia Uganda kama wakimbizi.
Mamia ya watu wamekimbia kutoka vijiji vya kivu kaskazini, mashariki mwa Congo, ambapo kuna utajiri mkubwa wa madini.
Mapigano makali pia yanaendelea katika sehemu za Kavumu na Shanghai, Rutshuru karibu a mpaka wa Bunagana, Uganda.
Waasi wa M23 wanapigana na wanajeshi wa serikali, ikiwa ni chini ya mwezi mmoja tangu viongozi wa jumuiya ya Afrika mashariki walipokutana jiji Nairobi, Kenya kuanzisha mazungumzo ya kuleta amani na kutaka kundi la M23 na makundi mengine ya silaha kuweka chini silaha mara moja. Viongozi hao vile vile walikubaliana kuunda kikosi cha jeshi kukabiliana na nawaasi hao.
Katika mahojiano na sauti ya Amerika mwezi uliopita, msemaji wakudi la M23 Meja Willy Ngoma, alisema kwamba wapiganaji hao walikuwa wanajibu “uchokozi wa wanajeshi wa serikali ambao walishambulia ngome zao.”
Willy Ngoma alisema kwamba “wanachotaka ni serikali ya DRC kuheshimu mkataba wa amani uliosainiwa Nairobi wakati wa utawala wa rais Joseph Kabila, mwaka 2013.”
Mkataba huo uliahidi wapiganaji wa M23 kujumulishwa katika jeshi la taifa, na baadhi ya viongozi wake kupata nafasi serikalini.