Rais Magufuli aapishwa kuongoza tena Tanzania

Rais John Pombe Magufuli (kushoto) akiapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamis Juma kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha pili cha Awamu ya Tano leo tarehe 05 Novemba 2020 katika sherehe zilizofanyika katika uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.

Rais Mteule John Magufuli Alhamisi ameapishwa kuiongoza tena Tanzania baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu nchini humo juma lililopita.

Magufuli anaingia katika kipindi cha pili cha uongozi wake huku akitaka taifa hilo kuungana pamoja baada ya uchaguzi wakati upinzani nchini humo ukitangaza kutotambua ushindi wake.

Katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma, makao makuu mapya ya serikali kwa mara ya kwanza linafanyika tukio la kuapishwa Kiongozi mkuu wa Nchi.

Katika hotuba yake Rais Magufuli amesisitza umuhimu wa Watanzania kuungana pamoja baada ya uchaguzi kumalizika

Wakati huohuo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan naye amekula kiapo kwa nafasi hiyo katika sherehe hizo. Tafrija hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya Nchi Wakiwemo Marais Yoweri Museveni wa Uganda, Emerson Mnangagwa wa Zimbabwe na Rais wa Comoro Azali Ossoumani.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan