Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Januari 27, 2025 Local time: 06:01

Upinzani Tanzania wataka jumuiya ya kimataifa kutotambua matokeo ya uchaguzi


Tundu Lissu
Tundu Lissu

Inatarajiwa kwamba Magufuli atapata ushindi mkubwa, na chama chake cha CCM kupata viti vingi bungeni

Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu ametaka jumuiya ya kimataifa kutotambua matokeo ya uchaguzi mkuu wa Tanzania, kwa madai kwamba umejaa dosari chungu nzima.

Tundu Lissu, ambaye ni mshindani mkuu wa rais wa sasa John Magufuli, ameambia waandishi wa habari kwamba matatizo yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi yana maana kwamba matokeo yake hayawezi kuaminika.

“Taasisi za kimataifa kama umoja wa Afrika, SADEC, Jumuiya ya Afrika mashariki na taasisi za kimataifa, zisitoe matangazo kwamba kulikuwa na uchaguzi hapa. Zitoe taarifa za kweli kuhusu hiki ambacho kimefanyika. Zisije zikatoa baraka kwa mchakato ambao ni haramu.” amesema Tundu Lissu, akiongezea kwamba “Jumuiya ya kimataifa na nchi rafiki wa Tanzania vile vile zisije zikakubaliana na hiki ambacho kimefanyika leo.

Mgombea huyo ametaka jumuiya ya kimataifa kuchukua “hatua kusaidia watanzania kwa kuwaadhibu hawa ambao wameharibu uchaguzi huu kwa njia mbalimbali. Hawa ambao wameshiriki moja kwa moja.”

Miongoni mwa wale ambao Lissu anataka waadhibiwe na jumuiya ya kimataifa ni Pamoja na maafisa wa tume ya uchaguzi, mkuu wa polisi, mkuu wa idhara ya usalama wa taifa miongoni mwa wengine.

Amesema kwamba amemwaagiza wakili wake kuasilisha ombi kwa mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya uhalifu dhidi ya binadamu ICC, ili wafanye uchunguzi kuhusiana na ripoti za watu kuuawa na polisi wakati wa kampeni hasa visiwani Zanzibar.

Lissu amesema kwamba hakubali kabisa matokeo ya kura hizo, akisema kwamba mchakato mzima wa maandalizi wake ulikuwa na makosa, ikiwemo kuzuiwa kufanya kampeni katika baadhi ya sehemu za nchi na wagombea wa upinzani kuenguliwa na tume ya uchaguzi kutoka kwa orodha ya wagombea.

“Hatukubaliani na chochote ambacho kimefanyika na matokeo yoyote. Watanzania ndio walioibiwa haki yao ya kuchagua na tumesema mara nyingi sana kwamba hatutakubali chochote ambacho sio uchaguzi huru, wa haki n aunaokubalika.” Amesema Lissu.

Kulingana na matokeo ya awali yanayotangazwa na shirika la habari la taifa - TBC, wagombea kadhaa wa chama kikuu cha upinzani CHADEMA wamepoteza karibu viti vyao vyote bungeni.

Kulingana na shirika hilo la utangazaji la serikali, miongoni mwa waliopoteza nafasi zao ni mwenekiti wa chama cha Chadema Freeman Mbowe ambaye kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, uchaguzi wa jumatano ulijaa vurugu na udanganyifu mkubwa katika hesabu ya kura.

Shirika la habari la taifa TBC, limesema pia kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT-wazalendo Zitto Kabwe naye ameshindwa kutetea nafasi yake bungeni.

Maafisa wa tume ya uchaguzi hawajatoa taarifa kuhusu madai ya Lissu na wenzake kutoka vyama vya upinzani, lakini Jumatano, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya uchaguzi Semistocles Kaijage alisema kwamba tume hiyo haijapokea malalamiko yoyote kuhusu kura bandia, na kuwataka Watanzania kupuuza taarifa hizo.

Mitandao ya kijamii hasa twitter, whatsapp, Instagram na you tube, imeminywa nchini humo na kuathiri mawasiliano.

Rais John Magufuli, ambaye ametimiza umri wa miaka 61 leo Alhamisi Octoba 29, anatarajiwa kuendeleza utawala wake na chama cha CCM.

Inatarajiwa kwamba Magufuli atapata ushindi mkubwa, na chama chake cha CCM kupata viti vingi bungeni.

Magufuli ameahidi kuimarisha ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Katika muhula wake wa kwanza, ameimarisha ujenzi wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa barabara, reli, mabwawa ya kuzalisha umeme, shirika la ndege la taifa miongoni mwa mengine.

Hata hivyo amekosolewa sana na makundi ya kutetea haki za kibinadamu na wanasiasa wa upinzani kwa kukandamiza haki za kibinadamu, upinzani na uhuru wa vyombo vya habari.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG