Rais John Pombe Magufuli ametangazwa rasmi kama mshindi wa uchaguzi mkuu wa Tanzania kwa kupata asilimia 84 ya kura ambayo ni sawa na kura 12,516,252 ya kura zote zilizopigwa Jumatano.
Mshindani wake wa karibu Tundu Lissu wa chama cha Chadema alipata kura 1,933,271. Kulingana na Tume ya Uchaguzi (NEC) watu waliojitokeza kupiga kura ni zaidi ya nusu kidogo ya watu 29,754,699 waliojiandikisha kupiga kura .
Kwa ushindi huu Rais Magufuli amepata awamu ya pili ya uongozi wa miaka mitano na chama chake cha CCM kimeendeleza utawala wake katika nchi hiyo tangu kupata uhuru miaka 59 iliyopita.
Akitangaza rasmi matokeo hayo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage alisema “John Magufuli ndio mshindi wa uchaguzi, amepata kura nyingi halali kuliko wagombea wengine, amechaguliwa kuwa rais wa Tanzania na Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu wa Rais.”
Chama cha CCM pia kimejipatia ushindi mkubwa katika bunge la Jamhuri ya Muungano na nafasi za udiwani katika halmashauri za nchi hiyo. Hadi idadi ya mwisho itakapotoka bunge la Tanzania huenda likawa na zaidi ya asilimia 90 ya wanachama wa CCM.