Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Novemba 04, 2024 Local time: 21:06

NEC wamkabidhi Rais mteule Magufuli cheti cha ushindi


Rais Magufuli akabidhiwa cheti cha ushindi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jumapili, Novemba 1, 2020. Picha na Global Publishers TV.
Rais Magufuli akabidhiwa cheti cha ushindi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jumapili, Novemba 1, 2020. Picha na Global Publishers TV.

Rais John Pombe Magufuli ameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kufanikisha uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020 na kubainisha kuwa baada ya kuibuka na ushindi ataliongoza taifa la Tanzania kwa miaka mingine mitano na ndio itakuwa ya mwisho.

Rais amesema hayo Jumapili Novemba Mosi, 2020 mjini Dodoma baada ya kukabidhiwa cheti cha ushindi na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage.

Magufuli amewashukuru Watanzania kwa ushindi huo na kusema ana deni kubwa la kuwalipa kwa imani kubwa walioionyesha kumchagua tena kuliongoza taifa hilo kwa miaka mingine mitano.

“Napenda kuipongeza sana Tume yetu ya Taifa ya Uchaguzi, kwa usimamizi mzuri wa uchaguzi wa mwaka huu asanteni sana, hakuna shaka kwa mtu yeyote aliyeshiriki ama kushuhudia, atakubaliana nami kwamba uchaguzi huu umefanyika vizuri sana tena kwa kiwango cha juu”

“Kwa namna pekee nashukuru na kuwapongeza Watanzania kwa kuonyesha ukomavu wa siasa na utulivu mkubwa katika kipindi chote cha uchaguzi, tulianza na kukamilisha kampeni kwa usalama. Tulipiga kura kwa usalama na tumepokea matokeo kwa amani na utulivu mkubwa”

“Mmetupa ushindi mkubwa sana ambao umetuachia deni kubwa sana, ninamuomba Mungu anisaidie katika kipindi hiki cha pili tuweze kukidhi haja za watanzania,” amesema Rais Magufuli ambaye ameshinda uchaguzi kwa kura 12,516,252.

Rais Magufuli ameeleza ushindi huo siyo wake peke yake wala wa chama chake bali ni wa watanzania wote. Amesema atawatumikia wote bila kujali wanapotoka, dini au kabila.

Amewapongeza baadhi ya wagombea wenzake kwa kukubali matokeo na kwenda kushiriki hafla hiyo akisisitiza kuwa ni ishara ya kukomaa kwao kisiasa.

“Tutajitahidi kuzingatia maoni yenu hasa yale yenye lengo la kuiletea Tanzania maendeleo,” amesema kiongozi huyo.

XS
SM
MD
LG