Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya watu laki saba hawana makazi ya kuishi kutokana na mafuriko mabaya kuikumba Sudan Kusini, janga lililojirejea kwa miongo kadhaa.
Takriban watu 40 wamekufa kote nchini wakati mvua kubwa na mafuriko yasiyokuwa ya kawaida yakiharibu mifugo, mashamba na nyumba za watu.
Majimbo ya Jonglei na Unity ndiyo yaliyoharibiwa vibaya, ikiwa ni asilimia 58 kati ya yale yaliyoathiriwa, shirika la msaada wa dharura limesema.
Wafanyakazi wa misaada wanatumia mitumbwi na boti kuwafikia watu waliokwama huku zaidi ya theluthi mbili ya maeneo yaliyoathiriwa sasa wanakabiliwa na hatari ya njaa.
Hali hiyo imepelekea bei za vyakula kuzidi kuongezeka kufikia asilimia 15 tangu mwezi Agosti.
Wanasayansi wameeleza kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yamesababisha mafuriko Sudan Kusini na nchi nyingine za Afrika Mashariki.