Amesema inakutana na Benki ya Dunia na Shirika la Kimataifa la Fedha ili kuzunguzmia juu ya utekelezaji wa mkataba wa amani wa Sudan Kusini wa mwaka 2018 na kutaka msaada wao.
Aliyasema hayo katika mahojiano na mwandishi wa Sauti ya Amerika Nabeel Biajo hapa washington DC.
Makamu wa Rais alizungumzia jumuiya ya kimataifa kutoridhishwa na maendeleo ya kisiasa nchini Sudan Kusini ambayo yamepelekea kuwekwa tena kwa marufuku ya silaha pamoja na vikwazo kwa baadhi ya watu binafsi.
“Siji hapa kukanusha kile kilichotokea nchini au kujitetea kwa kinachoendelea, ndio tunayo matatizo na kwa ugumu huu tunaokabiliana nao watu wetu wanategemea mengi kutoka kwenye serikali na kinachotokea kwa miaka mingi hakiwezi kubadilika kwa usiku mmoja. Ni utaratibu, tunawasihi watu wetu kuwa wavumilivu na sisi na serikali ya ushirikiano wa madaraka, sio sehemu moja, au mbili au tatu, kuna sehemu nyingi kwa hiyo sio rahisi kushawishi kila mmoja."
Aliongeza kuwa : "Kila kitu lazima kifanyike kufuatana na makubaliano ya mkataba kwa hiyo kama upande mmoja hauna furaha inachukua muda kwa matokeo kujitokeza. Ndio najua mkataba uko taratibu lakini tupo katika mwelekeo mzuri.”
Pia amezungumzia kuhusu kujumuisha wanawake katika serikali ya Sudan, na kusema :“Katika ofisi yangu Pamoja na ofisi nyingine kama vile wizara ya jinsia, watoto na masuala ya kijamii na bunge liliapishwa lakini kwa pamoja tunafanya kazi kuona uwakilishi wa wanawake unatambuliwa."
Pia ameeleza : "Ndio kuna matatizo kwa mfano, katika utawala kuna asilimia 26 na tunatakiwa tuwe na asilimia 35 na pia katika bunge lakini hatujafikia, tunazungumza ili kile ambacho hakijafikiwa katika maeneo mengine kifikiwe, najua tuna tatizo hilo lakini cha muhimu kwetu hivi sasa ni kwa watoto wetu kuwa salama na amani ipatikane nchini.”