Huduma za internet huko Sudan Kusini zilifungwa Jumatatu na vikosi vya usalama vilipelekwa mitaani, ambako kulikuwa kumetulia kuliko kawaida huku wakaazi wakijifungia ndani baada ya wanaharakati kuitisha maandamano dhidi ya Serikali ya Rais Salva Kiir.
Huku Kiir akipanga kuwahutubia wabunge katika kikao cha ufunguzi wa bunge Jumatatu asubuhi, muungano wa vikundi vya wanaharakati ulirudia wito wao Jumapili wa maandamano ya umma wakimtaka ajiuzulu.
Hata hvyo, hakukuwa na ishara yoyote mapema leo Jumatatu ya mikusanyiko barabara kuu katika mji mkuu wa Juba. Baadhi ya wanaharakati waliiambia Reuters walikuwa wamejificha kwa sababu za kiusalama.
Polisi walisema wanaharakati hawajaomba idhini ya kuandamana, na hivyo maandamano yoyote makubwa yatakuwa haramu.