Marehemu Maalim Seif azikwa kijijini kwao Pemba

Mwili wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ukiwasili katika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar ukitokea Jijini Dar es Salaam.

Aliyekuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amezikwa Alhamisi kisiwani Pemba.

Mazishi yake yamehudhuriwa na mamia ya Wazanzibar wakizungumzia namna gwiji huyo wa siasa za mageuzi alivyofanikisha kuwaacha Wazanzibar wakiwa wamoja.

Wananchi wajitokeza katika dua ya kuuaga mwili wa Maalim Seif, Unguja.

Mamia ya wananchi wa Kisiwa cha Unguja na Pemba kutoka maeneo mbalimbali walijitokeza hapo awali katika Viwanja vya Mnazi Mmoja kuuaga mwili wa aliyekuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Mallim Seif Sharif Hamad na baadaye kujitokeza kumzika kijijini kwake Mtambwe Pemba, Zanzibar.

Maalim Seif alifariki dunia Jumatano katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Maziko ya Maalim Seif kijijini Mtambwe Pemba yalihudhuriwa na Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi na viongozi wengine wa kitaifa kutoka Tanzania bara na visiwani.

Rais Hussein Mwinyi akiwa na viongozi wa serikali kuupokea mwili wa marehemu Maalim Seif ulipowasili Unguja, Alhamisi.

Watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa walimzungumzia namna Maalim Seif alivyokuwa na nia ya dhati ya kuleta umoja kwa wazanzibar na hata kukubali kuingia katika serikali ya Umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana

Mapema jijini Dar es Salaam Mufti Sheikh Abubakar Zubeir Bin Ali aliwaongoza mamia ya waombolezaji katika Swala na Dua ya KumuombeaMarehemu Maalim Seif Sharrif Hamad katika Msikiti wa Maamur uliopo Upanga,

Wakati huo huo mwili wa aliyekuwa katibu Mkuu kiongozi Balozi John Kijazi umewasili jijini Dar es Salaam kutokea Dodoma ambako alifariki dunia jana usiku.

Ibada ya kuuaga mwili wa Katibu Mkuu Kiongozi ambaye pia alikuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma itafanyika Ijumaa jijini Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa kuelekea Korogwe, Tanga kwa mazishi yanayotarajiwa kufanyika Jumamosi.