Naibu mwenyekiti wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo visiwani Zanzibar Nassor Mazrui ameachiwa huru kwa dhamana baada ya kushikiliwa na polisi tangu siku ya pili baada ya uchaguzi mkuu hapo tarehe 28 Octoba. Mazrui ameachiwa pamoja na Ayub Bakari Hamad siku moja kabla ya kusikilizwa kesi yao leo ya kutaka kuachiliwa huru. Akizungumza na Sauti ya Amerika kutoka hospitali mjini Nairobi, Ismail Jusa afisa muandamizi wa ACT Wazalendo aliyeumizwa wakati walipokamatwa Oktoba 29, anasema ni jambo zuri kwa Zanzibar na hivi sasa wataendelea na juhudi zao kudai haki kufuatia uchaguzi ambao anasema ulikua na wizi mkubwa wa kura.