Pia kiongozi huyo ameonya kuwa Libya inakabiliwa na "changamoto kubwa" ambazo zinaweza kudhoofisha uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi Desemba.
Akihutubia mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa Mataifa wa viongozi wa dunia mjini huko New York, hapa Marekani, Mohammed al-Menfi alisema mkutano huo utakusudia kuhakikisha "umoja, thabiti" wa msaada wa kimataifa na kurudisha hali ya uongozi, na umiliki wa mustakabal wa nchi hiyo.
Uchaguzi wa kitaifa, uliopangwa kufanyika Desemba 24, ulikusudiwa kumaliza mgogoro wa muda mrefu wa Libya, lakini mchakato huo umeingizwa kwenye majibizano makali kuhusu uhalali wake, hali ambayo huenda ikasambaratisha juhudi za amani za miezi kadhaa.
Menfi alikiri mbele ya viongozi wa dunia kwamba "Libya inapitia kipindi kigumu."
Waziri wa Mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian aliwaambia waandishi wa habari huko New York Jumatatu kwamba Ufaransa, Ujerumani na Italia zitashiriki mkutano wa kimataifa juu ya Libya mnamo Novemba 12 ili kuhakikisha kalenda ya uchaguzi itabaki vile ilivyo.