Kremlin yasema Putin amekutana na mkuu wa kikundi cha Wagner

Mkuu wa Kikundi cha Wagner Yevgeny Prigozhin na Rais wa Russia Vladimir Putin

Kremlin ilisema Jumatatu kuwa Rais wa Russia Vladimir Putin alikutana na mkuu wa Kikundi cha Wagner Yevgeny Prigozhin na makamanda kadhaa wa Wagner siku kadhaa baada ya Prigozhin kuongoza uasi wa kijeshi wa muda mfupi.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema mkutano huo wa saa tatu ulimhusisha Putin akitoa tathmini yake “ya matukio ya Juni 24,” siku ya uasi huo, na kuwasikiliza makamanda wakitoa maelezo yao ya kile kilichotokea.

Peskov alisema makamanda waliahidi kuendelea kupigana kwa ajili ya Russia.

Wagner imeshiriki katika uvamizi wa Russia nchini Ukraine, na Prigozhin alikuwa ameukosoa uongozi wa jeshi wa Russia kabla ya uasi, ambapo vikosi vya Wagner vilikamata kwa muda makao makuu ya kituo cha jeshi cha Russia cha upande wa kusini.

Uasi huo ulimalizika kwa makubaliano yaliyosimamiwa na Rais wa Belarus Alexander Lukashenko, na kumruhusu Prigozhin na wapiganaji wake kuhamia Belarus.

Rais wa Belarus Alexander Lukashenko

Uasi huo ulizua uvumi kwamba Rais wa Russia Vladimir Putin atafanya mabadiliko ya uongozi wake wa kijeshi.

Wizara ya Ulinzi ya Russia ilisambaza video siku ya Jumatatu ikimuonyesha Mkuu wa Wanajeshi Valery Gerasimov, jenerali wa ngazi ya juu wa nchi hiyo, akijitokeza kwa umma kwa mara ya kwanza tangu uasi huo kufanyika.

Video hiyo inaonyesha Gerasimov akipokea ripoti na kutoa amri kwa vikosi vya anga vya Russia na huduma za upelelezi wa kijeshi.

Gerasimov alikuwa mmoja wa walengwa wakuu wa ukosoaji wa Prigozhin, pamoja na Waziri wa Ulinzi Sergei Shoigu.

Bado akiwa hajaonekana hadharani ni naibu wa Gerasimov, Jenerali Sergei Surovikin, ambaye alikuwa na mahusiano ya muda mrefu na Prigozhin.

Habari hii inatokana mashirika ya habari ya AP, AFP, na Reuters