Kenya yatoa Shs 1.3 milioni kuwasaidia wanafunzi waliokwama Wuhan

Wafanyakazi wakifunga mboga katika mifuko katika soko la Wuhan, China.

Serikali ya Kenya imeeleza kuwa imetoa shilingi milioni 1.3 za matumizi kwa wanafunzi mia moja wanaoishi jijini Wuhan nchini China ambako kuna idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona.

Aidha, Wizara ya Afya nchini humo imetoa ombi kwa Wizara ya Fedha kutaka kutolewa kwa shilingi bilioni 1.8 kujengwa kituo cha kukabili virusi hivyo katika hospitali ya Mbagathi jiijini Nairobi.

Serikali ya Kenya imekuwa chini ya shinikizo la kuongeza tahadhari na kuwaondoa raia wake ambao ni zaidi ya wanafunzi 100 jijini Wuhan nchini China ambako vifo vingi vinavyotokana na maambukizi ya virusi vya corona vimeripotiwa.

Tahadhari hiyo imepelekea kusitishwa safari za mara tatu kwa wiki zinazofanywa na shirika la ndege la Kenya Airways, Kenya na wakati huohuo imeendelea kudhibiti watu wanaoingia Kenya kwa kuwakagua wasafiri kupitia viwanja vyake vya Ndege.

Kenya mara kadhaa imesisitiza kuwa haitawarudisha nyumbani raia wake walioko China, na iwapo itafanya hivyo, huenda itakuwa inahatarisha mamilioni ya raia wake.

Balozi wa Kenya jijini Beijing Sarah Serem amenukuliwa na vyombo vya habari akieleza kuwa hali inayowagubika Wakenya hao iko mikononi mwa Mungu.

Alhamisi, Msemaji wa serikali ya Kenya Cyrus Oguna amevieleza vyombo vya habari jijini Nairobi kwamba Kenya bado haijaafikia uamuzi wa kuwarejesha nyumbani raia wake waliokwama Wuhan.

Katibu wa Kudumu wa Wizara ya Fedha Julius Muia ameieleza Kamati ya bunge la Kenya kuhusu Fedha kuwa imepokea ombi kutoka kwa Wizara ya Afya kutolewa kwa shilingi bilioni moja nukta nane kujenga kituo cha kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona.

Pia itatumia fedha hizo kuwaondoa wanafunzi 100 kutoka Wuhan.

Katibu Mkuu : "Tumekuwa tukipokea mapendekezo ya kutoa shilingi bilioni 1.8 kuwaondoa wanafunzi wetu kutoka Uchina na vile vile kujenga kituo cha matibabu kando ya barabara ya Mbagathi kuwatenga na kuwafanyia vipimo vya kiafya,”

Haijafahamika iwapo hii ndio ishara ya Kenya kuridhia shinikizo la kuwaondoa raia wake kutoka Wuhan. China imeripoti kupungua kwa kasi maambukizi mapya ya virusi hivyo ambavyo vimesababisha vifo vya watu zaidi ya elfu mbili.

Japo kuwa Kenya imesema kwamba imeimarisha uwezo wake wa kuwatambua wale wanaogua kutoka maambukizi haya, Jumatano wabunge wa bunge la Seneti wametilia shaka uwezo wa Kenya kukabili virusi hivyo.

Mpaka sasa Kenya imeripoti kesi 13 zinazoshukiwa lakini ambazo hazijathibitishwa kuwa za maambukizi ya ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, dalili za ugonjwa huu wa Corona ni pamoja na kupungukiwa nguvu mwilini, joto jingi, kikohozi kilicho kikavu na kuwa na vidonda vya koo pamoja na kuwa na matatizo ya kupumua vizuri.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennedy Wandera, Kenya.