Rais Trump alitoa hotuba yake bila ya kutaja mashtaka dhidi yake katika Baraza la Seneti ambalo Jumatano linatarajiwa kupiga kura ya kufutilia mbali mashtaka hayo.
Katika hotuba yake Trump alizingatia zaidi masuala ya ndani ya nchi akilenga kutoa wito kwa wapiga kura kabla ya uchaguzi mkuu baadae mwaka huu.
Rais Trump alianza hotuba yake juu ya hali ya taifa katika mwaka wa uchaguzi 2020 kwa kukumbushia ahadi zake za kampeni alizotoa 2016.
Marekani kwanza
Rais Trump alisema : "Miaka mitatu iliyopita tulianzisha kampeni ya kuifanya Marekani kuwa taifa kuu tena. Hii leo ninasimama mbele yenu kuwaelezeni mafanikio makubwa tuliyoyapata."
Rais alionesha wazi mvutano uliyopo kati yake na Spika wa Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi kwa kutosalimiana naye alipowasili katika ukumbi wa Bunge kabla ya kuanza hotuba yake.
Alieleza kuwa hakuna shaka serikali yake imepata mafanikio ya kiuchumi ambayo alisema wademokrat wanapinga.
Gavana wa Jimbo la Michigan Gretchen Whitmer alijibu hotuba ya Rais akikana madaia ya rais kwamba mpango wa Wademokrat wakupanua mpango wa huduma za afya kugharimiwa na serikali ni mapinduzi ya kisoshalisti.
Gretchen Whitmer, Gavana wa Jimbo la Michigan
Whitmer alisema kila Mdemokrati anaegombania kiti cha rais ana mpango wa kupanua huduma ya afya kwa Wamarekani wote.
"Kila mtu ameunga mkono huduma ya afya ya Obama Care kuwahudumia watu wote. Huenda mipango yao inatafautiana lakini lengo ni sawa. Lakini Rais Trump kwa bahati mbaya ana mpango tofauti, anaomba mahakama kufutilia mbali huduma muhimu za kuokoa maisha," amesema.
Matayarisho ya uchaguzi
Akiwa anajitayarisha kwa ucahguzi wa mwaka 2020, Trump anafurahia uchunguzi mpya wa maoni unaompatia kiwango cha juu cha kufanya kazi cha asilimia 49 tangu kuingia madarakani.
Hata hivyo alizungumzia pia ushirikiano wake na China na mikataba ya biashara na mafanikio yake ya kigeni, iIkiwa ni pamoja na kumualika mgeni maalum Rais wa Venezuela anaetambuliwa na Marekani Juan Guaido.
Rais ameeleza kuwa Wamarekani wameungana na wavenezuela katika vita vya kupata uhuru wao.
Trump aliwahakikishia pia Wamarekani kwamba serikali inashughulikia mlipuko wa virusi vya Corona.
Ushirikiano na China
Trump amesema : "Tunashirikiana na serikali ya China na kufanya kazi kwa karibu pamoja kukabiliana na mlipuko wa virusi vya Corona huko China.
Utawala wangu utachukua hatua zote muhimu kuhakikisha usalama wa raia wetu kutokana na kitisho hicho."
Lakini wachambuzi wanasema rais hakuzungumzia sana juu ya ushirikiano wa kisiasa pamoja na wademokrats.
Na mchambuzi wa kisiasa wa chuo kikuu cha American Bill Sweeney anasema kutotaja kesi dhidi yake haimanishi kwamba hajakasirishwa na hali hiyo na mvutano uliyopo.
"Ni wazi kabisa ulipokuwa anatizama wabunge hukuwaona wademokrats wakimpigia makofi kuhusu masuala yanayohusiana na umoja wa taifa. Wakati huo huo hujamsikia akipendekeza kufanya kazi kwa pamoja pia, jambo ambalo ni kawaida kusisitiza katika hotuba yake juu ya hali ya taifa.
Trump na Pelosi hawajazungumza tangu mwezi Oktoba na ugomvi wao ulijidhihirisha wazi hapo jana.
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.