Wengi wa wanawake hao wanaotoka katika jamii maskini wanatoa wito wa kutambuliwa kutokana na mchango wao licha ya maisha magumu wanayoyapitia.
Wakati dunia inaadhimisha siku ya wanawake. Fatma Said amezungukwa na mawazo hajui mlo wake wa kesho unatokea wapi.
Fatma ni mjane anayetegemewa na familia hivyo analazimika kufanya kazi ngumu ili kuweka chakula mezani.
Lakini kadri siku zinavyosonga mbele, Fatma hawezi tena kufanya kazi.... amelazimika kutegemea majirani wanaompa chakula cha kujipikia nyumbani.
“Mimi sina mzee, mimi ndio Mama, mimi ndio baba, mimi ndio dada mkubwa kwetu. Si unajua kusumbuana na watu wengine ni shida, kwa sababu maisha yamekuwa magumu hao pia wanshida zao. Sasa inabidi mwenyewe ujipiganie .kitambo nilikuwa nauza samosa na gharama ya maisha ilikuwa chini, saa hizi unga gano ni shilingi 200, mafuta shilingi 210, makaa shilingi 80 na hakuna faida ninayopata,” anasema Fatma.
Wanawake wengi kama Fatma wanaofanya kazi za kipato cha chini katika jamii ,hawana ufahamu wowote wa umuhimu wa siku ya Kimataifa ya Wanawake i ambayo maadhimisho yake hufanyika katika miji na maeneo mengine ya mijini.
Fatma anasema hajui ni kwa nini na Siku ya Wanawake huadhimishwa ikiwa wale wanaotoka katika jamii maskini hawaangaziwi.
Fatma anasema yeye hana la kujivunia kwa sababu hajui maana ya siku ya wanawake, wala hajawahi kuhushishwa huwa anaona tuu kwa TV kina mama warembo, kina mama wasafi wanakwenda kwenye sherehe, “lakini sisi tunakaa kuangalia TV na kujionea meza zimejaa vyakula vya kila aina huku mimi nikijiuliza pahali nitatoa Sukuma.”
Hali ni sawia kwa Mama Esther Nyagweso, licha ya kuwa ana mume, amebeba mzigo wa familia kwa kufanya vibarua zaidi ili kuhakikisha familia yake inapata lishe kwa siku. Maisha yamekuwa magumu kwake kila kukicha anawaza jinsi atakavyo kwenda mashambani, yeye kulekea mashambani ni heri kuliko kuishi maisha magumu mjini.
“Leo amekataa kwenda kazi, yeye mwenyewe. Sasa nikauliza kwa hii nyumba hatuna chakula, hatuna hata sukari tunafanyaje? Nina mtoto mdogo, sasa akitaka maziwa nitafanya nini, sasa mimi nafanya kazi na namuambia nikipata pesa nitakwenda mashambani, kwa sababu haya maisha ninayopitia ni magumu ,” anasema Esther Nyagweso
Madhimisho ya siku ya wanawake yanajiri huku wanawake wakibeba mzigo mzito kwa kuiangalia familia, baadhi ya wanawake wakijitahidi kuwajiri kinamama zaidi mitaani ilikuwasaidia wajikimu kimaisha.
Esther anaelezea zaidi hali ilivyo “sasa mimi ndio mama na Baba, nikipata tule nikikosa tukae hivi hivi tu.”
Ni wazi kuwa Fatma na wanawake wengine nchini Kenya wameathiriwa na gharama ya juu ya maisha , mzigo wa kulisha familia na hata kutafuta matibabu kwa ajili ya watoto.
“Maisha ya kila siku ... ukiamka asubuhi ukae mlangoni , pengine mtu akuite njoo unisafishie nyumba au nioshee vyombo upate riziki yako ya shilingi 100 na hiyo mia moja pengine unataka ujipange, huna sukari, hauna unga, hauna makaa na hauna maji na hiyo shilingi mia moja haina thamani, Ukikosa unamashukuru mola maana yeye ndiye mpaji lakini maisha yamekuwa magumu sana,” Fatma anasema.
Ingawa wanawake wengi wamejitahidi kujikwamua kutokana na gharama ya maisha, wengine katika maeneo yaliyokumbwa na ukame bado wanajikaza kwa kutafutia familia zao chakula.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu Hubbah Abdi, VOA Nairobi.