Mahusiano ya watu wa jinsia moja ni kinyume cha sheria katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika na adhabu yake ni kifungo cha hadi miaka 14 jela.
Wanawake hao wanne, wenye umri wa kati ya miaka 22 na 29, wameshtakiwa kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kwa maafisa wa umma na kufanya mkutano usio halali, alisema msemaji wa polisi Danny Mwale katika taarifa yake.
“Washukiwa wako chini ya ulinzi wa polisi na watafikishwa mahakamani hivi karibuni,” alisema Mwale .
Watuhumiwa hao wanaoshikiliwa na polisi ni pamoja na mwanzilishi mwenza na wanachama wengine wawili wa Taasisi ya Sistah Sistah, shirika lisilo la kiserikali ambalo Jumapili liliandaa maandamano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia katika mji mkuu wa Lusaka, kabla ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Jumatano.
Siku ya Jumatatu, serikali ya Zambia ilisema maandamano hayo yalitumiwa "kutetea maswala yasiyo halali na ya kihalifu."
Taarifa hiyo imelaani kile ilichokiita tabia ya "kutowajibika" ya wale waliohudhuria mkutano huo, ambapo walikuwa wakiimba wakiwa wamebeba mabango ya "kuunga mkono ushoga".
"Serikali inapenda kuukumbusha umma kwamba kama taifa la Kikristo, wana wajibu wa kuzingatia tabia zenye maadili ya Kikristo na kibinadamu," msemaji wa serikali Chushi Kasanda alisema katika taarifa yake.
Picha za tukio hilo zilizobandikwa kwenye mitandao ya kijamii ziliwaonyesha dazeni ya watu wakiandamana mjini humo, baadhi wakiwa wamebeba mabango yenye maandishi yaliyosomeka “Hapana ni hapana” na “Hakuna kanuni za mavazi kwa ubakaji”.
Katika picha moja mwanamke alionekana akiwa ameshika bendera ndogo yenye upinde wa mvua, huku picha nyingine ikimuonyesha mhudhuriaji mmoja akiwa amevaa barakoa yenye upinde wa mvua.
Zambia kwa muda mrefu imekuwa ikipinga wito wa kimataifa wa kuondoa sheria zinazopinga haki za watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja, licha ya shinikizo kutoka kwa wafadhili ambao hutoa misaada muhimu
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari ka AFP.