Mswada unawalenga watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, wamiliki wa nyumba na hoteli, wamiliki wa vyumba vya burudani, mashirika yanaoyoeneza ushoga, waandishi wa habari, watengenezaji filamu miongoni mwa wengine.
Kwa mara nyingine tena, Uganda inajaribu kutunga sheria kali dhidi ya ushoga, mara hii mswada unalenga kila mtu anayechangia kwa namna yoyote kueneza mapenzi ya jinsia moja nchini humo.
Asuman Basalirwa, mbunge wa manispaa ya Bugiri, mashariki mwa Uganda, ambaye ameandaa mswada huo, ameambia Sauti ya Amerika kwamba mswada wake unalenga kuweka mazingira magumu kabisa kwa ushoga kufanyika Uganda, kwa kuwalenga wafadhini wa ushoga, wanaoeneza, wamiliki wa hoteli, vyumba vya burudani na wenye nyumba za kawaida za kukodisha.
Adhabu kwa watakaovunja sheria
Wanaoneza ushoga kwa kuchapisha vitabu, na wafadhili, watatozwa faini ya shilingi milioni 100 za Uganda. wanaomiliki vyumba vya kufanyia ushoga watahukumiwa miaka 7 gerezani huku wamiliki wa nyumba watakaokodisha kwa watu walio katika uhusiano wa mapenzi ya jinsia moja watahukumiwa mwaka mmoja gerezani.
Mtu yeyote atakayejaribu kushawishi mwingine kufanya mapenzi ya jinsia moja atafungwa miaka 5 gerezani na atakayepatikana na makosa ya kusimamia au kubariki ndoa hizo atafungwa miaka 10 gerezani.
Waandishi wa habari, wahariri, watengenezaji filamu watakaofichua waathiriwa wa ushoga bila idhini yao watatozwa faini ya shilingi milioni 5.
Sheria ya mwaka 2014 dhidi ya mashoga ilifutwa na mahakama
Mswada wa Asuman hata hivyo una adhabu ndogo ikilinganiswa na mswada uliopitishwa na bunge mwaka 2014, kusainiwa na rais Yoweri Museveni kuwa sheria na baadaye kufutwa na mahakama kwa msingi kwamba wakati ulipokuwa unapitishwa, hakukuwa na idadi ya wabunge wanaohitajika kupitisha mswada bungeni. Sheria hiyo ilikuwa na adhabu ya Maisha gerezani.
Asuman, anasema kwamba ushoga unaenezwa na watu wanaochapisha vitabu na kufadhili vitendo hiyvo, mambo ambayo hakuna sheria katika sheria za sasa za Uganda kushughulikia hilo.
Viongozi wa dini nchini Uganda, saw ana rais Yoweri Museveni wamesema kwamba hawatakubali vitendo vya ushoga nchini humo. Msimamo kama huo vile vile umechukuliwa na serikali za Kenya na Tanzania.