Palma ulitekwa katika shambulizi lililopangwa hapo Machi 24, ikiwa kusambaa kwa uasi ambao umeendelea kupamba moto katika Jimbo la Cabo Delgado kwa zaidi ya miaka mitatu.
Jumapili, Jeshi hilo liliwasindikiza maafisa na waandishi wa habari kwenda mjini Palma.
Kamanda Chongo Vidigal, kiongozi wa operesheni za kijeshi za kuukomboa mji wa Palma, ameiambia televisheni ya serikali TVM kuwa eneo hilo hivi sasa liko “salama”, licha ya kusita kutangaza kuwa jeshi limepata udhibiti kamili wa mji huo.
“Eneo la uwanja wa ndege ni sehemu pekee tuliyohitaji kulidhibiti na tulifanya hivyo asubuhi ya leo. Ni sehemu salama kabisa,” Vidigal alisema.
“Nafikiri kuwa ni idadi kubwa ya magaidi waliouawa,” amesema, akiongeza kuwa mamlaka zitatoa idadi kamili baadae.
Maelfu wameukimbia mji huo wenye wakazi 75,000 ambapo darzeni ya raia waliuawa, kulingana na idadi iliyotolewa na serikali hapo awali, na kampuni kubwa ya nishati ya Total imeondoka katika eneo ambapo mradi wa gasi uliogharimu mabilioni ya dola unaendelezwa.
Picha za video zilionyesha wanajeshi wakifunua maiti kutoka kwenye mifuko ya plastiki katika mitaa hiyo.
Picha nyingine zilionyesha mabaki ya majengo yalioungua, ikiwemo mabenki, hospitali na ofisi ya mwendesha mashtaka wa serikali.