Jenerali wa Marekani: 'Wanajeshi zaidi ya 100,000 wa Russia wauawa Ukraine'

Jenerali Mark Milley

Jenerali wa ngazi ya juu wa jeshi la Marekani alikadiria Jumatano kuwa jeshi la Russia limeshuhudia zaidi ya wanajeshi wake 100,000 kuuawa na kujeruhiwa nchini Ukraine na kuongeza kuwa majeshi ya Kyiv “huenda” yamekabiliwa na kiwango kama hicho cha vifo katika vita.

Makadirio hayo hayakuweza kuthibitishwa na vyanzo huru vya shirika la habari la Reuters.

Lakini matamshi ya Jenerali Mark Milley inatoa makadirio ya juu kabisa ya Marekani ya vifo hivyo kufikia leo katika vita vilivyodumu kwa miezi tisa na imekuja wakati ambapo Ukraine na Russia wanakabiliwa na uwezekano wa kusitisha mapigano ambayo wataalam wanasema huenda yakatoa fursa ya namna fulani ya mashauriano.

Akiulizwa kuhusu matarajio ya kutumia diplomasia nchini Ukraine, Milley alieleza kuwa kukataa awai kuingia katika mazungumzo wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia kuliongeza madhila makubwa kwa wanadamu na kupelekea vifo vya mamilioni ya watu.

“Hivyo, kunapokuwa na fursa ya mashauriano, wakati amani inaweza kufikiwa … chukua fursa hiyo,” Milley aliiambia Klabu ya Uchumi ya New York.

Mapema Jumatano, Russia ilitangaza kuwa majeshi yake yataondoka kutoka ukingo wa magharibi wa Mto Dnipro karibu na mji wa kimkakati wa Kherson ulioko kusini mwa Ukraine, katika hatua kubwa ya kuelemewa kwa Moscow na uwezekano wa kubadilisha mwelekeo wa vita.

Baadhi ya wataalam wanasema hatua hii ya kurudi nyuma kwa Moscow inaweza kuipa fursa Ukraine kufanya mashauriano ikiwa sehemu yenye nguvu wakati wengine wanatoa hoja kwamba Russia inaweza kutumia mashauriano hayo ili kuvuta muda kubadilisha na kusawazisha majeshi yake kwa ajili ya kufanya mashambulizi kipindi cha majira ya machipuko.

Milley alisema kuwa viashiria vya awali vinaeleza kuwa Russia ilikuwa inaendelea na utaratibu wake wa kuondoa majeshi kutoka Kherson. Lakini alitahadharisha kuwa inaweza ikachukua muda kukamilika.

“Haitawachukua siku moja au mbili, hii itawachukua siku kadhaa na pengine wiki kadhaa kuondosha majeshi yao kusini mwa ziwa hilo,” Milley alisema, akikadiria kuwa huenda Russia ina idadi ya wanajeshi 20,000 hadi 30,000 kaskazini mwa Mto Dnipro katika eneo hilo.

Washirika wa Ukraine ambao ni Marekani na NATO hawakuingilia moja kwa moja katika vita vya Ukraine, lakini wanatoa silaha, ushauri na kuliwezesha jeshi la Ukraine kuilinda Kyiv dhidi ya uvamizi wa majeshi ya Russia.

Milley alisema vita hiyo hadi sasa imepelekea Waukraine kati ya milioni 15 na 30 kuwa wakimbizi na kuuliwa takriban raia 40,000 wa Ukraine.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Reuters.