Mzozo kati ya waasi wa M23 na wanamgambo watiifu kwa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo umeongezeka katika jimbo la mashariki la Kivu Kaskazini tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba, hasa kaskazini mwa mji mkuu wa jimbo hilo, Goma.
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya uhamiaji limesema watu wengi ambao wamekimbia makaazi yao lakini walibaki ndani ya mipaka ya DRC wanahitaji sana msaada ili kukidhi mahitaji yao ya msingi.
“IOM inaongeza juhudi zake za kushughulikia mgogoro wenye utata unaoendelea nchini DRC wakati idadi ya wakimbizi wa ndani (IDPs) ikiongezeka hadi watu milioni 6.9 nchini kote, idadi kubwa zaidi iliyorekodiwa”, ilisema taarifa hiyo.
“Kwa migogoro inayoendelea na kuongezeka kwa vurugu, DRC inakabiliwa na moja ya migogoro mikubwa ya ndani na ya kibinadamu duniani”.