Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya (EU) Urusla von der Leyen Jumatano ameitisha mkutano wa wafadhili mbalimbali utakaofanyika Mei 4, kuchangia fedha kwa ajili ya utafiti wa kutengeneza na kusambaza ulimwenguni chanjo dhidi ya COVID-19.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa Habari uliofanyika kupitia teknolojia ya video huko Brussels, Von der Leyen ameiita chanjo itakayopatikana “ ni njia bora ya pamoja katika kutokomeza virusi vya corona.”
Rais huyo amesema kongamano hilo pia litachangia kwa ajili ya kuboresha matayarisho ya majanga na pia kuchochea shughuli za upimaji na matibabu.
Amesema wakati ikipatikana chanjo, kitachofuatia ni wao kushughulikia jinsi gani ya kusambaza hiyo chanjo duniani kote.
Von der Leyen amesema kongamano hilo litaandaliwa nchini Brussels lakini litaendeshwa kwa njia ya mtandao na nchi zitatoa ahadi ya michango yao.
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.