DRC: Watu zaidi ya 100 wahofiwa kufariki katika mafuriko makubwa Kinshasa

Mafuriko mjini Kinshasa Januari 4, 2017. ( Picha na VOA/TopCongo)

Inasadikiwa watu zaidi ya 100 wanahofiwa kufariki katika mafuriko makubwa yaliyotokea katika mji mkuu wa Kinshasa huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Inaelezewa kuwa mvua kubwa zimesababisha mafuriko mabaya sana. Idadi hiyo inaelezewa huenda ikaongezeka wakati serikali inaendelea na juhudi za uokoaji.

Maelfu ya watu wamekoseshwa makazi, taarifa iliyotolewa na serikali imesema.

Barabara kuu katikati ya Kinshasa, jiji lenye watu milioni 15 zilifurika, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

Picha zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha maporomoko ya ardhi katika wilaya ya Mont-Ngafula, yakiikata barabara kuu namba 1, njia kuu ya usafirishaji wa bidhaa inayounganisha mji mkuu na bandari ya Bahari ya Atlantiki ya Matadi.

Mafuriko yalifurika pia barabara katika wilaya ya Gombe ambako kunapatikana soku kuu, wizara za serikali na afisi za balozi.