Mwanachama wa pili wa kundi la kupambana na ulaji rushwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Ghislain Muhiwa amekamatwa baada ya kumtuhumu mke wa Rais Felix Tshisekedi kwa ubadhirifu wa mali ya umma.
Kundi la vijana la kupigania mageuzi, maarufu kama Lucha, linatuhumu kwamba taasisi inayoisimamiwa na mke wa Rais, Denise Tshisekedi, imepora msaada uliyokuwa umelengwa kuwapa waathiriwa wa mlipuko wa volcano katika mlima Nyiragongo, mashariki wa nchi DRC.
Taasisi ya mke wa Rais imekanusha tuhuma hizo.
Mtuhumiwa alikamtwa akiwa anaelekea kupeleka mahari kwa wakwe zake mjini Goma.
Mwenzake Parfait Muhani alikamatwa mwezi Julai kwa madai hayo hayo anasubiri kesi yake mbele ya mahakama ya kijeshi.