Dalai Lama awataka watu kuchukua chanjo dhidi ya COVID-19

Kiongozi wa kiimani wa Tibet, Dalai Lama akipatiwa chanjo katika kituo cha chanjo cha Dharamsala, India, Machi 6, 2021. (Office of his holiness the Dalai Lama/Handout via Reuters)

Kiongozi wa kiimani wa Tibet, Dalai Lama, ameisihi dunia kuwa shujaa na kuchukua chanjo dhidi ya COVID-19.

Kiongozi huyo aliyasema hayo Jumamosi baada ya kudungwa chanjo ya virusi vya Corona katika mji wa kaskazini mwa India wa Dharmsala.

Hata hivyo, vyanzo vya habari vinasema baadhi ya nchi zinapata shida kupata chanjo za kutosha kwa watu wake.

Khofu ya kuhodhi chanjo imeanza kuibuka, kufuatia habari kwamba Italia imezuia shehena ya chanjo za AstraZeneca kwenda Australia.

Ripoti ya shirika la habari la AP inasema kuwa Umoja wa Ulaya umepanga kuiomba Washington kuhakikisha kuwa nchi za EU zinapata mamilioni ya dozi za chanjo za AstraZeneca ambazo bado wanazihitaji, pamoja na vitu vinavyohitajika katika kutengeneza chanjo.

"Tunaamini tunaweza kufanya kazi pamoja na Marekani," tume ya Ulaya imesema katika taarifa yake.