Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 05:33

Kenya imepokea shehena ya kwanza ya chanjo dhidi ya COVID-19


Chanjo ya AstraZeneca inayotumika dhidi ya COVID-19
Chanjo ya AstraZeneca inayotumika dhidi ya COVID-19

Waziri wa afya Kenya, Mutahi Kagwe ameihakikishia nchi yake dawa zaidi zitawasili na hakuna haja ya kuogopa. “Hii ni shehena ya kwanza, kutakuwa na chanjo zaidi zinakuja na hivyo hatutaki mtu yeyote kuogopa na kufikiri kwamba hawatapatiwa chanjo

Kenya Jumanne ilipokea chanjo milioni moja ya virusi vya Corona kutoka Oxford na AstraZeneca, taifa la kwanza la Afrika mashariki kupokea chanjo hiyo. Wizara ya Afya nchini humo imesema itatenga dozi laki nne za virusi vya corona kwa wafanyakazi wa huduma za afya nchini humo.

James Kamau akiwa katika umri wa miaka ya 60, ni mmoja kati ya mamilioni ya wakenya wanaoishi na HIV. Ni baba wa watoto wawili anafurahia kuhusu chanjo za COVID-19 zinazowasili nchini humo. “Nikipewa fursa hiyo, nitafanya hivyo kwa sababu ni faida kwangu kwamba ninapatiwa chanjo. Kama nilichomwa chanjo ya BCG bila kuulizwa nab ado ina faida, basi sioni sababu kwa nini nisichomwe hii pia. Hapa nilipo nina kinga zaidi kuliko watu wa kawaida, na inapendekezwa sana watu kupata chanjo. Ni kweli, hatujui madhara yatakayotokea, lakini kwa maoni yangu, faida ya chanjo ni kubwa kuliko athari ya kutopatiwa chanjo”

Kenya imepokea shehena yake ya kwanza ya chanjo ya virusi vya Corona siku ya Jumanne. Takribani wafanyakazi wa afya laki nne watapewa kipaumbele katika upewaji chanjo, ikifuatiwa na wazee pamoja na watu wenye hali ya matatizo sugu ya kiafya, kama vile Kamau.

Kenya inakadiriwa kuwa na watu milioni 50 kwa hivyo dozi milioni moja ni mwanzo tu.

Waziri wa afya Kenya, Mutahi Kagwe
Waziri wa afya Kenya, Mutahi Kagwe

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea chanjo hiyo kwenye uwanja wa ndege Waziri wa afya Kenya, Mutahi Kagwe ameihakikishia nchi dawa zaidi zitawasili na kwamba hakuna haja ya kuogopa. “Hii ni shehena ya kwanza pekee, kutakuwa na chanjo zaidi zinakuja na kwa hivyo hatutaki mtu yeyote kuogopa na kufikiri kwamba hawatapatiwa chanjo. Jambo la pili ni kwamba hili ni zoezi la hiyari, sio chanjo ya kulazimishwa. Watu ambao wanataka kupatiwa chanjo watapewa na tunatumai kwamba wengi wanahitaji hii chanjo”.

Kenya inakuwa mojawapo ya nchi chache za kiafrika ambazo zimepokea chanjo ya virusi vya Corona.

Catherine Kyobutungi ni mkuu wa kituo cha utafiti wa idadi ya watu na afya barani Afrika. Anasema changamoto kubwa kwa Afrika ni kupata dozi za kutosha kushinda dhana potofu na upotoshaji kuhusu chanjo hii. “Lakini kwa mtu aliye mtaani wakati mwingine ni ngumu kutofautisha kati ya teknolojia tofauti ambazo zimetumika kutengeneza chanjo. Kwa hivyo kuna maoni mseto iwapo chanjo ni salama au la, ama ilitengenezwa haraka sana kuliko ilivyotarajiwa. Lakini chanjo zote zimepitia majaribio magumu, usalama na ufanisi wao umeidhinishwa na serikali ambayo pia imeweka mifumo sahihi ya kuhakikisha kuwa ni sahihi na inafaa kwa matumizi ya nchi”.

Takribani serikali kote ulimwenguni zimeidhinisha chanjo hizo na kuwahimiza raia wao kupatiwa chanjo.

Kufikia sasa zaidi ya watu milioni 50 nchini Marekani wamepatiwa angalau dozi ya kwanza ya chanjo ya Pfizer au Moderna.

Mfano wa virusi vya COVID-19
Mfano wa virusi vya COVID-19

Kenya ilirekodi kesi yake ya kwanza ya virusi vya Corona mwezi Machi mwaka jana. Kufikia sasa zaidi ya watu laki moja wameambukizwa virusi vya Corona na angalau watu 1,000 wamekufa.

Taifa hilo la Afrika mashariki bado lipo kwenye kipindi cha muda wa kutotoka nje wakati wa usiku na serikali ilipiga marufuku mikutano ya hadhara ili kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo.

XS
SM
MD
LG