COVID-19 : Uingereza yaweka katazo dhidi ya wasafiri kutoka Uganda

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson

Uingereza imeiongeza Uganda kwenye orodha ya mataifa ambayo wasafiri wake hawataruhusiwa kuingia nchini humo, kuanzia tarehe 30 mwezi huu.

Haya yanajiri wakati ambapo maambukizi ya aina mpya ya virusi vya Covid 19, yanaongezeka kwa kasi nchini Uganda.

Hadi sasa, Uganda imekuwa kwenye orodha ya nchi ambazo raia wa Uingereza walikuwa wametahadharishwa kutotembelea.

Lakini sasa ni wakazi tu na raia wanaorejea watakaoruhusiwa kuingia nchini Uingereza, kuanzia Jumatano wiki ijayo.

Uganda inapambana na wimbi jipya la janga la Corona, na idadi ya maambukizi na vifo imekuwa ikiongezeka kwa kasi tangu mwishoni mwa mwezi Mei.

Rais Yoweri Museveni alitangaza Ijumaa kuwa siku ya mapumziko ili kufanya maombi ya kitaifa na kuomboleza na familia, ambazo zimewapoteza wapendwa wao kutokana na ugonjwa huo.

Habari hii inatokana na vyanzo mbalimbali ikiwemo VOA News