Clinton, Bush, Obama kuhudhuria ibada ya mazishi ya shujaa Lewis

Watu wahudhuria Ibada ya kumbukumbu ya John Lewis katika Bunge la Marekani, Washington DC Julai 27, 2020. (Matt McClain/The Washington Post via AP, Pool)

Shujaa Mwakilishi wa Baraza la Wawakilishi John Lewis atazikwa Alhamisi baada ya ibada ya maziko yake huko Atlanta.

Marais wastaafu Barack Obama, Bill Clinton na George W. Bush wanatarajiwa kuwa kati ya waombolezaji watakaohudhuria mazishi katika Kanisa la Ebenezer Baptist, eneo la kihistoria ambapo Martin Luther King Jr. alikuwa akihubiri.

Marais wastaafu Barack Obama, George W. Bush, na Bill Clinton.

Obama anatarajiwa kuzungumza katika ibada hiyo ya kumuaga Lewis.

Baada ya hapo Lewis atapelekwa kuzikwa katika eneo la makaburi ya South View mjini Atlanta.

Marehemu alikufa wiki iliyopita kutokana na saratani akiwa na umri wa miaka 80.

Lewis alitumikia Baraza la Wawakilishi kwa miaka 33 akiwa ni mwakilishi kutoka wilaya ya uwakilishi ya tano ya jimbo la Georgia inayoijumuisha Atlanta.

Waombolezaji walijipanga katika mitaa mbalimbali katika njia ambapo gari lililokuwa limeubeba mwili wa Lewis lilipita Jumatano likiupeleka mwili wa marehemu katika jengo la bunge.

Watu wengi walisimama katika mistari mirefu kutoa heshima zao mbele ya jeneza lililokuwa limefunikwa kwa bendera, wakati muda wa kutoa heshima uliongezwa zaidi ili kuwawezesha wale wote waliotaka kutoa heshima zao kufanya hivyo.

Katika hafla hiyo, Gavana wa Georgia Brian Kemp alisema Lewis “alikuwa kipenzi cha watu wa Georgia,” shujaa wa Marekani na rafiki kwa wale wote waliokuwa wanataka maisha bora, haki, na jamii iliyokuwa na mshikamano zaidi.”

Ibada ya Alhamisi ndio inahitimisha wiki nzima ya maadhimisho ya kuenzi maisha ya Lewis.

Mwili wake ulipitishwa Jumapili katika daraja la Selma, Alabama ambapo akiwa kijana mwaka 1965 alikuwa kati ya waandamanaji wanaodai haki za kiraia waliopigwa na askari wa jimbo hilo.

Mwili wa Lewis uliwekwa katika Bunge la Marekani Washington kwa siku mbili kabla ya kuondoshwa na kupelekwa Georgia kwa mazishi.