Kuchaguliwa tena kwa waziri mkuu kunaimarisha muelekeo wa kimataifa wa ushindi wa vyama vyenye mrengo wa kulia vilivyokuwa na wafuasi wengi, kuanzia Marekani hadi Brazil , Italia, na hilo hutokea baada ya kuweka msimamo mikali ya kulinda masoko yao, uhamiaji na ulinzi.
Takwimu zilizotolewa na Tume ya Uchaguzi zinaonyesha kuwa Chama cha Modi Bharatiya Janata kinaongoza kwa viti 302 kati ya viti 542 ikiwa ni idadi ya juu Zaidi kuliko ushindi wa viti 282 walioupata mwaka 2014 na zaidi ya viti 272 vinavyotakiwa kwa chama kuwa na uwingi katika baraza kuu la Bunge.
Matokeo hayo yanakipa chama chake ushindi wa viti vingi kwa mara nyingine kwa chama kimoja tangu mwaka 1984. Kura zitahisabiwa kikamilifu siku ya Ijumaa asubuhi.
Modi alishangiliwa kwa kutupiwa maua na maelfu ya wafuasi wake waliokuwa wanafuraha ambao walimsubiri kwa masaaa kadhaa katika mvua awasili katika makao makuu ya chama Alhamisi jioni.