Blinken aitaka China kutumia ushawishi wake kuleta utulivu Mashariki ya Kati

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alitoa wito Jumamosi kwa China, mshirika wa Iran, kutumia ushawishi wake kuleta  hali ya utulivu katika Mashariki ya Kati.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani, ambaye alikuwa akizuru Saudi Arabia, alifanya mazungumzo ya simu "yenye tija" ya saa moja na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Matthew Miller alisema.

"Ujumbe wetu ulikuwa kwamba anadhani ni kwa manufaa yetu pamoja kuzuia mzozo huo kuenea," Miller aliwaambia waandishi wa habari kwenye ndege iliyombeba Blinken kutoka Riyadh kuelekea Abu Dhabi.

"Alidhani inaweza kuwa muhimu ikiwa China inaweza kutumia ushawishi wake."

China ina uhusiano mzuri na Iran, ambayo uongozi wake unaunga mkono Hamas, kundi la Kiislamu la Palestina linalotawala Gaza, ambalo lilifanya mashambulizi makali ndani ya Israel wiki moja iliyopita, na Hezbollah, kundi la wanamgambo wa Lebanon ambalo pia huenda likaanza makabiliano na Israel.

Wang kwa upande wake alisema kuwa Marekani inapaswa "kuchukua jukumu lenye tija na la kuwajibika, katika kurejea kwa suluhu la kisiasa haraka iwezekanavyo," kulingana na wizara ya mambo ya nje ya China.

"Wakati wa kushughulika na masuala ya kimataifa, nchi kubwa lazima zifuate usawa, kudumisha utulivu na kujizuia, na kuongoza katika kuheshimu sheria za kimataifa," alisema Wang.