Baraza la Wawakilishi Marekani latarijiwa kupitisha mswaada wa afueni

Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi

Baraza la Wawakilishi la Marekani, Jumatano linatarajiwa kupitisha mswaada unaoungwa mkono na Rais Joe Biden, wa kuwapa Wamarekani kiasi cha dola trilion 1.9, kwa lengo la kuzisaida familia, na pia kuimarisha biashara.

Spika wa baraza hilo Nancy Pelosi, amesema ana uhakika mswaada huo utapitishwa, na kwamba lengo lake kuu ni "kuokoa maisha ya Wamarekani na kuwapa watu matumaini ya siku zijazo."

Wabunge wa Republican wamepinga mswaada huo, wakisema kiasi hicho cha pesa ni kikubwa mno, na kwamba hakiwalengi ipasavyo, wale wanaohitaji sana, msaada wa kiuchumi.

Kiongozi wa Wachache kwenye Baraza la Wawakilishi Kevin McCarthy, jana aliutaja mswaada huo kuwa wenye gharama kubwa, na uliogubikwa na rushwa.”

Mswaada huo ulipitishwa katika Seneti Jumamosi, bila uungwaji mkono kutoka kwa Warepublican, baada ya kubadilishwa kwa vipengele kadhaa, vilivyokuwa vimepitishwa na baraza la wawakilishi hapo awali.

Miongoni mwa mabadiliko hayo ni kuondolewa kwa pendekezo la nyongeza ya kiwango cha chini cha mishahara kwa Wamarekani.