Kauli yake hiyo imekuja siku moja baada ya ripoti mbalimbali za Wizara ya Nishati ya Marekani kuhitimisha kuwa kuna uwezekano kuwa mlipuko wa ugonjwa huo ulianza kwenye maabara nchini China zilivujisha virusi hivyo.
Nicholas Burns alieleza hayo katika hafla ya Baraza la Biashara la Marekani kwa njia ya video Jumatatu kuwa China inahitaji kuwa “wakweli zaidi kuhusu nini kilitokea miaka mitatu iliyopita huko Wuhan ambako ndiko chanzo cha mgogoro wa COVID-19.” Wuhan ni mji wa China ambako maambukizi ya kwanza ya virusi vya corona viliripotiwa mwezi Desemba 2019.
Maoni yake yamekuja siku moja baada ya vyombo vya habari vya Marekani kuripoti kuwa Wizara ya Nishati ilibaini kuwa janga hilo kuna uwezekano lilitokana na kuvuja kwa virusi katika maabara iliyoko Wuhan.
Wizara ilitoa uamuzi katika ripoti ya siri ya kipelelezi iliyopelekwa White House na viongozi wa Bunge, kwa mujibu wa Jarida la The Wall Street, ambalo hapo awali iliripoti maendeleo hayo, ikiwataja watu waliosoma ripoti hiyo.
Jarida la WSJ lilisema kitengo cha upelelezi cha Wizara ya Nishati hivi sasa ni kitengo cha kiintelijensia cha pili cha Marekani baada ya Shirika la Upelelezi la FBI, kukata shauri kwamba maabara ya China iliyovujisha virusi ilikuwa pengine ndio sababu ya janga hilo, ingawaje mashirika ya kijasusi ya Marekani yamegawanyika juu ya chanzo cha virusi hivyo.
Msemaji wa usalama wa taifa White House John Kirby alikubaliana na hisia hizo.
“Hapakuwa na hitimisho la moja kwa moja na makubaliano katika serikali ya Marekani kuhusu chanzo cha janga la COVID-19,” Kirby aliwaambia waandishi Jumatatu alipoulizwa kuhusu ripoti ya WSJ.