Mapema mwezi huu wakazi wa kitongoji kimojawapo cha Johannesburg cha Alexandra, waliandamana wakilalamika juu ya maisha mabaya na kusema hawatoshiriki kwenye uchaguzi Mei 8, 2019.
Wakati huohuo Rais Cyril Ramaphosa anaegombea muhula wake wa kwanza anaahidi mageuzi makubwa.
Rais Ramaphosa
Lakini Rais Cyril Ramaphosa anasisitiza kuwa : Ni lazima tujibu machungu na maisha magumu wanaoshuhudia watu wetu hapa. Hata hivyo wakazi wengi hapo hawaamini mambo yatabadilika.
Chama cha ANC kilichoko madarakani tangu uhuru wa Afrika Kusini 1994, kina viti 249 sawa na asilimia 62 ya viti 400 vya bunge. Wakati Chama kikuu cha upinzani cha DA kina asilimia 22.
Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa bado chama cha ANC kinaamini kuwa upinzani sio tishio kwa chama tawala.
Kampeni zapamba moto
Wakati kampeni zikipamba moto kabla ya uchaguzi wa Mei 8, 2019, wakazi wengi wa Alexandra hawana imani tena na chama tawala cha African National Congress na wengine hawana pia imani na chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance kilichochukua udhibiti wa jiji la Johanesburg tangu 2016.
Kero za wananchi
Johanna Ditsela mkazi wa kitongoji hicho anasema huwenda hatopiga kura.
"Mimi ninahitaji kazi na ninahitaji nyumba kwa ajili ya watoto wangu , ili niweze kuwalea katika nyumba yenye hadhi nilikuwa na matumaini kwamba siku moja nitakapofariki nitawaachia wanangu makazi ya heshima," amesema..
Ditsela mwenye umri wa takriban miaka 50 ameishi katika kitongoji cha Alexandria kwa miaka 30 katika nyumba ya mabati pamoja na watoto wake watano kando ya mtaro wa maji machafu.
NontsikeleloThinto mkazi mwengine wa kitongoji hicho anasema hata Ramaphosa akiwatembelea hatoweza kuleta mabadiliko yeyote
Anaeleza kuwa : "Ramaphosa inabidi atuambie kile tunachotakiwa kufanya. Angalia mahali ninapoishi. Hiki ni kibanda cha chumba kimoja na ninaishi na watoto wangu . kwa mfano mtoto moja akitaka kukoga inatulazimu tutoke nje, mumewangu akikoga watoto wanatoka nje. Maisha gani haya na sote hatuna kazi."
Juhudi za Ramaphosa
Ramaphosa amekuwa akihudhuria kampeni usiku na mchana kuwarai wapiga kura milioni 27 kumpatia nafasi nyingine na kukichagua chama chake cha ANC.
Katika kampeni zake kiongozi huyo aliyechukuwa madaraka baada ya aliyemtangulia Jacob Zuma kulazimika kuacha madaraka kutokana na kashfa za rushwa mwaka 2018, amekuwa akiahidi nyumba mpya, kompyuta mashuleni na maisha bora.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC