Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 12:21

Waziri Mkuu wa Haiti ajiuzulu, baraza la mpito kuelekea uchaguzi laundwa


Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry

Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry amejiuzulu kama kiongozi wa taifa la Caribbean, kiongozi wa jumuiya ya kikanda na rais wa Guyana alisema Jumatatu usiku.

Henry, daktari wa upasuaji wa neva mwenye umri wa miaka 74 amekuwa akishililia nafasi hiyo ambayo siyo ya kuchaguliwa, tangu mauaji ya mwaka 2021 ya rais wa mwisho wa nchi hiyo, Jovenel Moise.

"Tunatambua kujiuzulu kwake baada ya kuanzishwa kwa baraza la rais la mpito na kumtaja waziri mkuu wa muda," alisema mwenyekiti wa Jumuiya ya Caribbean (CARICOM) Irfaan Ali, akimshukuru Henry kwa utumishi wake kwa Haiti.

Henry alisafiri hadi Kenya mwishoni mwa mwezi uliopita kujadili uongozi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki kwa ujumbe wa kimataifa wa usalama unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kusaidia polisi wa Haiti kupambana na magenge yenye silaha, lakini ongezeko kubwa la ghasia katika mji mkuu, Port-au-Prince, wakati wa kutokuwepo kwake lilimfanya kukwama kayika jimbo laPuerto Rico.

Ali alisema baraza la rais litakuwa na waangalizi wawili na wajumbe saba wa kupiga kura, wakiwemo wawakilishi kutoka miungano kadhaa, sekta binafsi, mashirika ya kiraia na kiongozi mmoja wa kidini.

Baraza hilo limepewa mamlaka ya "haraka" kumteua waziri mkuu wa muda, aliongeza, na yeyote ambaye ana nia ya kugombea katika uchaguzi ujao wa Haiti hataweza kushiriki.

Waandamanaji wawasha mioto kwenye mitaa ya Port au Price, Haiti.
Waandamanaji wawasha mioto kwenye mitaa ya Port au Price, Haiti.

Kujiuzulu kwa Henry kunajiri wakati viongozi wa eneo hilo walikutana mapema Jumatatu katika nchi jirani la Jamaica kujadili mfumo wa mpito wa kisiasa, ambao Marekani ilitka wiki iliyopita "uharakishwe" huku magenge yenye silaha yakitaka kupindua serikali yake.

Viongozi wa kanda, wakizungumza na wawakilishi kutoka sekta mbalimbali za jamii ya Haiti, wameangazia kuanzisha baraza la mpito linalonuiwa kufungua njia kuelekea uchaguzi wa kwanza tangu 2016.

Henry, ambaye raia wengi wa Haiti wanamchukulia kuwa fisadi, alikuwa ameahirisha uchaguzi mara kwa mara, akisema lazima usalama urejeshwe kwanza.

Muhula wa mwisho wa maseneta wa Haiti uliisha mwanzoni mwa 2023.

"Sote tunajua kwamba hatua za haraka zinahitajika katika safu za kisiasa na kiusalama," Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema mapema Jumatatu, akitoa wito wa kuundwa kwa "baraza la urais chenye makao yake makuu, jumuishi na huru."

Blinken alikuwa amesema baraza hilo litakuwa na jukumu la kukidhi "mahitaji ya haraka" ya watu wa Haiti, kuwezesha ujumbe wa usalama kutumwa na kuhakikisha hali ya usalama, ambao ni muhimu kwa uchaguzi huru.

Haiti ilitangaza hali ya hatari mwezi huu huku mapigano yakiharibu mawasiliano na kupelekea wafungwa kutoroka mara mbili kutoka gerezani baada ya Jimmy "Barbeque" Cherizier, kiongozi wa muungano wa makundi yenye silaha, kusema kwamba wangeungana na kumpindua Henry.

Blinken Jumatatu aliahidi msaada mwingine wa dola milioni 133 kwa Haiti, akisema mzozo uliokithiri nchini humo unaonyesha dharura ya kupeleka kikosi cha kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken.

Akihutubia mkutano wa dharura wa nchi za eneo la Caribbean huko Jamaica, Blinken alisema Marekani itatoa msaada mwingine wa dola milioni 100 kwa kikosi cha kimataifa na msaada mwingine wa kibinadamu wa mara moja wa dola milioni 33, na hivo ahadi za jumla za Marekani kwa Haiti zikiwa sawa na dola milioni 333.

Haiti imekumbwa kwa miongo kadhaa na umaskini uliokithiri, majanga na mzozo wa kisiasa lakini mambo yamekuwa mabaya zaidi tangu kuuawa kwa rais Jovenel Moise mwaka wa 2021.

Magenge ya wahalifu wenye silaha yanayodhibiti sehemu kubwa ya nchi na sehemu kubwa ya mji mkuu yalizidisha mashambulizi tangu wiki iliyopita.

Forum

XS
SM
MD
LG