Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Novemba 22, 2024 Local time: 20:07

Wavuvi Zanzibar wadai kodi nyingi ni hasara kwa biashara


Wavuvi wakiwa baharini wakati wa machweo huko Zanzibar. REUTERS/Radu Sigheti
Wavuvi wakiwa baharini wakati wa machweo huko Zanzibar. REUTERS/Radu Sigheti

Vijana Zanzibar wanasema mrundikano wa kodi katika sekta ya uvuvi unawafanya washindwe kufanya uvuvi yenye tija, na kuitaka serikali kuboresha miundo mbinu na kutafuta fursa zaidi ili kuwanufaisha vijana na uchumi wa bluu.

Vijana hao ambao huendesha maisha yao kupitia uvuvi, ukulima wa mwani, ujenzi wa viwanda vya samaki, pamoja na utalii wa fukwe na michezo ya baharini,

Wamedai kupitia changamoto mbalimbali ikiwemo mrundikano wa kodi, ushuru pamoja na changamoto katika kupata vibali kwa ajili ya kufanya shughuli hizo.

Adili Mansuri mmoja wa vijana anayejishughulisha na uvuvi visiwani Zanzibar amesema changamoto hizo zinawafanya kutumia nguvu nyingi katika kujipatia kipato, lakini kipato kinachopatikana kinaishia katika kulipa kodi na ushuru wa serikali.

“Nguvu ambazo unatumia katika kazi ili kukamilisha ndoto zako unakuta ile pesa unayoipata yote inaishia katika kulipa ushuru na kodi kwahiyo ni suala ambalo serikali inatakiwa iliangalie sana kwasababu hii ni sekta ya uvuvi ambayo inajiri sana vijana.” Alisema Mansuri

Idadi kubwa ya vijana Zanzibar wanajishughulisha na uvuvi ili kujiingizia kipato, baadhi yao wameiambia Sauti ya Amerika kuwa wanataka kuona ubunifu zaidi katika uchumi wa bluu ili kuibua maeneo mengine yenye fursa kwa vijana ambayo yatakayo wasaidia kupata ajira.

Mbali na matumizi bora ya rasilimali za baharini kuleta fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi wa Zanzibar, vijana wa Zanzibar wameitaka serikali kuangalia fursa nyingine zinazopatikana baharini ikiwemo madini.

Wavuvi wakiwasiri ufukweni katika soko la Samaki la Malindi, Zanzibar Desemba 28, 2017. Picha na GULSHAN KHAN/AFP.
Wavuvi wakiwasiri ufukweni katika soko la Samaki la Malindi, Zanzibar Desemba 28, 2017. Picha na GULSHAN KHAN/AFP.

“Kwa sasa sisi tunazalisha mwani peke yake lakini kwenye uchumi wa bluu kuna raslimali nyingi, kuna gesi, kuna uvuvi wa samaki tofauti tofauti kuna madini kama ya lulu,” alisema Abasi Mkazi wa Fuoni Zanzibar.

“Marjani inaweza kuwepo kwenye bahari zetu vilevile, kuna gesi asilia pamoja na zao la chumvi,” aliongeza.

Asilimia 90 ya wanawake wanaoishi pembezoni mwa bahari visiwani Zanzibar wanajishughulisha na kilimo cha mwani ambacho nacho bado hakijaleta manufaa kwa vijana kutokana na ukosefu wa viwanda vya kuchakata zao hilo kwa lengo la kutoa ajria kwa vijana.

Ally Mawazo kutoka visiwani humo ameiambia Sauti ya Amerika licha ya zao la mwani kuwa na faida kubwa bado serikali imeshindwa kujenga viwanda vya kuchakata zao hilo pamoja na kujenga viwanda vya kusindika samaki ambavyo kwa kiasi kikubwa vinaweza kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.

Alisema “zao la mwani lina faida kubwa sana lakini hatujakiona kiwanda cha mwani chenye kuleta faida na kuajiri vijana, hatujaona vifaa vya baharini vya kuvulia samaki pamoja na vifaa vya kusindika samaki.”

Uchumi wa Zanzibar kwa kipindi kirefu umekuwa ukitegemea zaidi katika sekta ya utalii pamoja na uchumi wa bluu suala ambalo wananchi visiwani humo wanaona ipo haja ya serikali kuongeza ubunifu zaidi ili kupata vyanzo vipya vya mapato vitakavyofungua nafasi za ajira kwa vijana na kuongeza pato la taifa.

Issa amesema serikali inapaswa kuanzisha miradi mbalimbali kupitia visiwa ambavyo vimekuwa havitumiki kwa kukaribisha wawekezaji katika visiwa hivyo ili waweze kujenga viwanda ambavyo vitasaidia kuchakata malighafi zinazopatikana visiwani humo zitakazouzwa kama bidhaa.

Wavuvi wakionyesha samaki zao katika kisiwa cha Pemba huko Zanzibar. Picha na Marco LONGARI / AFP
Wavuvi wakionyesha samaki zao katika kisiwa cha Pemba huko Zanzibar. Picha na Marco LONGARI / AFP

“Suala zima la ukodishaji wa visiwa vidogo vidogo ambavyo serikali haina uwezo wa kufanya chochote katika visiwa vile, inaweza kuanzisha miradi tofauti tofauti na wageni hawa wanaokuja kukodi hivi visiwa au wakajenga viwanda vidogo vidogo katika visiwa hivyo ili raslimali zinazotoka hapa yaani malighafi ziweze kusanifiwa hapa hapa kwetu halafu tuuze kama bidhaa.” Alisema Issa.

Hata hivyo bado vijana wanasema ukosefu wa miundo mbinu bora ya uvuvi na sekta nzima ya uchumi wa bluu kwa vijana umepelekea changamoto nyingi kwao ikiwemo ukosefu wa ajira ambao wakati mwingine umekuwa ukisababishwa na wastaafu kutokutoka makazini baada ya kumaliza muda wao.

Idirisa Mwadini anasisitiza wastaafu wanapaswa kutoka makazini ili kuwapisha vijana ambao wanakumbwa na tatizo kubwa la ajira kutokana wastaafu kurudishwa makazini wanapomaliza muda wao na hivyo kupelekea ugumu wa maisha kwa vijana visiwani humo.

“Ikitokea kazi hatuchukuliwi sisi vijana wanachukuliwa wao na mfano akishastaafu mtu sio kwamba anapumzika, bali anafanyiwa mpango anakwenda kufanyakazi sehemu nyingine najiuliza kwani wafanyakazi wengine hawapo,” alisema Mwadini na kuongeza “sasahivi kuna uzee wa Mungu na uzee wa kutengenezwa, kuna uzee wa kutengenezwa kwamba maisha ni magumu, unajikuna wala huwashwi kwa maisha magumu.”

Vijana hao wanasema licha ya kuendelea kupitia changamoto mbalimbali lakini bado hawana budi kufanya kazi japo kazi hizo zimekuwa na manufaa madogo kwao.

Imetayarishwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Zanzibar.

Forum

XS
SM
MD
LG