Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 22:32

Wapiga kura wajitokeza; wasiwasi juu ya utulivu DRC watanda


Wafanyakazi wa tume ya huru ya uchaguzi wakishusha vifaa vya kupigia kura, huku vyombo vya usalama vikiimarisha ulinzi huko Bukavu, Disemba 28, 2018.
Wafanyakazi wa tume ya huru ya uchaguzi wakishusha vifaa vya kupigia kura, huku vyombo vya usalama vikiimarisha ulinzi huko Bukavu, Disemba 28, 2018.

Uchaguzi wa rais na wabunge nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambao umecheleweshwa kwa muda mrefu hatimaye unafanyika Jumapili, lakini waangalizi wa uchaguzi wanatabiri kuwa kutakuwa na hali ya kutokuelewana na vurugu nchini humo.

Nchi yenye utajiri mkubwa wa madini, ambayo ni theluthi mbili ya ukubwa wa Ulaya magharibi lakini ina miundo mbinu michache, haijawahi kukabidhiana madaraka kwa amani katika miaka 60 ya kujitawala.

Ripoti za awali Jumapili zimesema kuwa vituo vingi havikuweza kufunguliwa wakati ambao uchaguzi ulitakiwa uanze.

Mchambuzi wa muda mrefu wa Congo Stephanie Wolters wa Taasisi ya Tafiti za Masuala ya Usalama anasema yeye hana wasiwasi sana na matokeo ya uchaguzi lakini ana wasiwasi na mazingira hatarishi ya uchaguzi ambayo zaidi ya wapiga kura 40 milioni wanaweza kukabiliwa nayo siku ya Jumapili.

“Nafikiri suala nyeti ambalo linatukabili hivi sasa ni kwamba kutakuwa na vurugu maeneo mengi Jumapili. Tunapokea ripoti zikionyesha namna maandalizi ya uchaguzi yaliyofanywa na tume ya uchaguzi (CENI) yalivyokuwa mabovu,” amesema mwanamama mchambuzi huyo.

“Vifaa vya kupigia kura havijapelekwa vituoni inavyopaswa; tunasikia kuwa ilivyo badala ya kuhisabu kura katika vituo, Tume huru ya uchaguzi itapeleka matokeo ya uchaguzi kutoka katika vituo kwa njia ya inteneti.

Tunasikitishwa na uhalali wa kiufundi wa jambo hili la kutuma matokeo kwa inteneti, juu ya uwezekano wa kutokea vurugu, na uwezekano wa kuwepo uvunjifu wa amani.”

Kuelekea uchaguzi huu kumekuwa na vurugu kama hizo. Ilikuwa uchaguzi ufanyike 2016, lakini serikali ikachelewesha mara kadhaa, wakidai kutokuwepo maandalizi. Hilo liliruhusu Rais Joseph Kabila kuendelea kuwa madarakani zaidi ya miaka miwili baada ya muhula wake kumalizika.

Mwaka 2018, Tume ya uchaguzi ya taifa ilitangaza kuwa uchaguzi utafanyika mwisho wa mwaka. Hilo pia limekumbwa na misukosuko.

Upande wa upinzani ulipaza sauti ukisema kuna mchezo mchafu juu ya machine za kupigia kura zenye utata zilizotengenezwa Korea, ambazo wamezielezea kuwa ni “machine za kuchakachua uchaguzi” ambazo zitawapa fursa muungano wa vyama tawala kuiba kura.

Kadhalika wiki iliyopita maafisa wa DRC walitangaza kuwa watachelewesha uchaguzi katika maeneo matatu yasio na utulivu -- ambayo pia yamekuwa ni maeneo muhimu ya upinzani na yana zaidi ya wapiga kura milioni 1 – kwa sababu ya wasiwasi juu ya uvunjifu wa amani na mlipuko wa maradhi ya Ebola.

Na wakati taifa linasubiri kwa hamu kupiga kura, baadhi ya waangalizi wa kura, kama vile Claude Kabemba, ambaye ni mkurugenzi wa taasisi ya Southern Africa Resource Watch yenye makao yake Johannesburg, amesema kuwa wao hawana matumaini.

Pamoja na kuwa kura za maoni za hivi karibuni zinaonyesha kuwa mgombea wa upinzani Martin Fayulu anaonyesha kuongoza katika kinyang’anyiro hicho, Kabemba anadiriki kusema kuwa Kabila yeye mwenyewe – na siyo mrithi wake aliyemchagua, Emmanuel Ramazani Shadary—ndiye ataibuka kidedea.

“Tunakoelekea ni kuwa Rais Joseph Kabila ataendelea kuwepo madarakani kwani huo ndio mkakati wenyewe, hiyo ndio fikra yenyewe, na ndio lengo la mbinu yote iliyofanyika,” amesema Kabemba.

Kabemba ameeleza kuwa ubabaishaji uliopo ni kwa Kabila “kuuonyesha ulimwengu kuwa, ‘tuko tayari kufanya uchaguzi, nimeandaa uchaguzi, wananchi wa Congo wametoa pesa, na tume huru ya uchaguzi imeundwa – kwamba hili limefanyika, kwamba hili limefanyika, kwamba hili limefanyika. Kwa sababu Katiba inasema lazima niendelee kuwa madarakani mpaka pale rais mpya atakapo apishwa, hivyo, nitaendelea kuwa madarakani.’ Huo ndio mkakati.”

XS
SM
MD
LG