Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 15, 2025 Local time: 16:41

Wanasheria Tanzania wadai mswaada utakaoleta mabadiliko ya katiba


Rais Samia Suluhu Hassan akikagua gwaride la heshima, baada ya kuapishwa kuwa rais wa kwanza wa kike Tanzania March 19, 2021. Picha na AFP.
Rais Samia Suluhu Hassan akikagua gwaride la heshima, baada ya kuapishwa kuwa rais wa kwanza wa kike Tanzania March 19, 2021. Picha na AFP.

Kituo cha sheria na haki za binaadamu kiimeitaka serikali kuwasilisha mswaada wa sheria wa kufanya mabadiliko ya katiba kutokana na baadhi ya marekebisho katika sheria hizo kushindwa kufanyika kutokana na mapungufu yaliyopo kwenye katiba ya nchi hiyo.

Kauli hiyo imefuatia hatua ya rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kusaini sheria mpya za uchaguzi za mwaka 2024, ambapo wanasheria hao wanadai kuwa sheria mpya zilizosainiwa zimeshindwa kutatua mapungufu ya muda mrefu ya katika katiba hiyo, ikiwemo kuendelea kwa watumishi wa umma kuwa sehemu ya tume ya uchaguzi.

Wameyataja mapungufu mengine ni pamoja na maamuzi ya tume na matokeo ya urais kutohojiwa mahakamani, na uwakilishi mdogo wa wanawake bungeni.

Wakili wa kujitegemea jijini Dar es Salaam, Tito Magoti aliiambia Sauti ya Amerika kuwa marekebisho yaliyopo yana mapungufu yanayoendelea kumpa nguvu rais aliyopo madarakani.

Wakili huyo alisema “Marekebisho haya yamejaribu kupaka rangi kile kilichokuwepo bila kuathiri kitu chochote kwa maana kwamba bado tume ya uchaguzi na watumishi wake wanateuliwa na rais jambo ambalo tulidhani kwamba halikuwa sawa na ni jambo kubwa sana ambalo linaamua matokeo ya uchaguzi,” alisema

Wafuasi wa Chama tawala cha CCM walipokusanyika katika uwanja wa Kibanda Maiti huko Zamzibar.
Wafuasi wa Chama tawala cha CCM walipokusanyika katika uwanja wa Kibanda Maiti huko Zamzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari, mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za binadamu, Anna Henga alieleza changamoto nyingine ambazo zimeshindwa kutatuliwa na sheria hizo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa wabunge na madiwani wanawake wa viti maalumu na suala la kuwepo kwa mgombea binafsi asiyehusiana na chama chochote cha siasa.

Naye ni mkurugenzi wa shirika la uraia na msaada wa kisheria (CILAO) Odero Odero amesema kukosekana kwa mgombea binafsi kuna wanyima haki Watanzania na kuwalazimisha kujiunga na chama cha siasa ili waweze kuwa viongozi.

“Bado Watanzania wanalazimishwa kwa nguvu kuwa wanachama wa vyama vya siasa ili waweze kuwa viongozi. Jambo hili lilisha amuliwa na mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu kwamba serikali ya Tanzania ilishapewa muda ifanyie marekebisho sheria yake” alisema, na kuongeza kuwa “Kwa hiyo, tulitarajia katika marekebisho haya katiba ingefanyiwa marekebisho ili kuruhusu raia yoyote ambaye ana umri unaotakikana kisheria kugombea.”

Wafuasi wa chama cha upinzani cha Wazalendo wakiandamana huko Zanzibar Oktoba 28, 2020..
Wafuasi wa chama cha upinzani cha Wazalendo wakiandamana huko Zanzibar Oktoba 28, 2020..

Wakili Henga ameitaka serikali kuwasilisha muswaada wa sheria utakaotoa fursa ya kufanya marekebisho ya katiba ili kuruhusu masuala yaliyoshindwa kufanyiwa marekebisho kutokana na mapungufu ya katiba kurekebishwa.

“Uwasilishwe muswaada wa sheria utakaotoa fursa ya kufanya mabadiliko ya katiba kwasababu bado kilio chetu sisi ni katiba ili kuruhusu baadhi ya masuala ambayo kwa uasili wake hayawezi kufanyiwa marekebisho bila kugusa katiba,” alisisitiza Henga.

Wakati wakili magoti akiwataka wananchi kujenga utaratibu wa kujihusisha katika mabadiliko mbalimbali ya sheria yanayoletwa na serikali ili kuchochea upatikanaji wa sheria bora.

Imeandaliwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika, Dar es Salaam

Forum

XS
SM
MD
LG