"Tumeanzisha msako wa kuwakamata wote waliohusika katika shambulio hilo la kikatili, miongoni mwao wakiwa wanajeshi waliopo kazini na wastaafu," msemaji wa jeshi Kanali Issa Bangura aliwaambia waandishi wa habari.
Hata hivyo shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa watu wamerejea katika shughuli zao za kawaida huku kukiwa na ulinzi mkali katika mji mkuu wa Sierra Leone, Freetown siku ya Jumatatu, wakati serikali ikiondoa kwa kiasi amri ya kutotoka nje iliyowekwa baada ya mapigano ya silaha kuzuka mjini humo.
Mapema siku ya Jumapili, washambuliaji waliokuwa na silaha walivamia ghala ya kijeshi na magereza kadhaa, na kusababisha mapigano na vikosi vya usalama yaliyodumu kwa saa kadhaa katika mji mkuu.
Sierra Leone ni nchi ya Afrika Magharibi inayozungumza Kiingereza, ambayo imekuwa ikipitia mzozo wa kisiasa kufuatia uchaguzi wa mwezi Juni.
Siku ya Jumatatu, serikali iliondoa amri ya kutotoka nje wakati wa mchana ambayo ilikuwa imewekwa na kuwataka watu warejee tena katika maisha yao ya kila siku huku wakiendelea kuwa macho.
Ilisema amri ya kutotoka nje itabaki kati ya saa tatu usiku na saa kumi na mbili asubuhi.
Mjini Freetown, baadhi ya maduka na benki zilifunguliwa na usafiri wa magari ulianza tena Jumatatu, lakini shule bado zimefungwa, kulingana na mwandishi wa habari wa AFP aliyeko katika jiji hilo.
Vituovya ukaguzi vimewekwa kwenye barabara kuu, ambapo wana usalama walikuwa wakipekua magari.
Wakati huohuo maswali mengi yalibakia kuhusiana nini kimetokea nchini humo, huku kukiwa na hofu ya kutokea mapinduzi mengine katika eneo hilo la Afrika Magharibi, ambapo Mali, Burkina Faso, Niger na Guinea zote zimekumbwa na misukosuko tangu 2020.
Chanzo cha habari ni Shirika la habari la Reuters
Forum