Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 21, 2024 Local time: 17:16

Waliberia wamchagua rais wao


Rais wa Liberia aliyepo madarakani George Weah na mpinzani wake mkuu Joseph Boakai. Picha na JOEL SAGET na Brendan SMIALOWSKI / AFP.
Rais wa Liberia aliyepo madarakani George Weah na mpinzani wake mkuu Joseph Boakai. Picha na JOEL SAGET na Brendan SMIALOWSKI / AFP.

Raia wa Liberia wamepiga kura siku ya Jumanne katika uchaguzi mkuu wa rais ambapo gwiji wa soka Rais George Weah anawania muhula wa pili, baada ya miaka sita yenye tuhuma za ufisadi na matatizo ya muda mrefu ya hali ngumu ya uchumi.

Amani ikiwa ni miongoni mwa masuala muhimu kwa wapiga kura katika taifa hilo ambalo liliharibiwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Takriban watu milioni 2.4 wanastahili kupiga kura katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa mbili asubuhi na kufungwa saa kumi na mbili jioni.

Tume ya uchaguzi itaanza kutoa matokeo siku ya Jumatano.

Ili kuepuka kurudiwa kwa uchaguzi, mshindi lazima apate asilimia 50 ya kura zilizopigwa, na angalau apate kura moja zaidi.

Wachambuzi wanaamini kuna uwezekano mkubwa kuwa uchaguzi huo unaweza kurudiwa ambapo Weah anaweza kushikilia madaraka.

Rais Aliyepo madarakani George Weah akipiga kura katika kituo cha kupigia kura mjini Monrovia Oktoba 10, 2023 Picha na GUY PETERSON / AFP
Rais Aliyepo madarakani George Weah akipiga kura katika kituo cha kupigia kura mjini Monrovia Oktoba 10, 2023 Picha na GUY PETERSON / AFP

Weah mwenye umri wa miaka 57, aliingia kwenye siasa baada ya kupata mafanikio katika soka akiwa mwanasoka wa kimataifa, na kumfanya kuwa Mwafrika wa kwanza na pekee kushinda tuzo ya mtu binafsi yenye hadhi kubwa sana ya kandanda, Ballon d'Or, mwaka 1995.

Amesema anahitaji muda zaidi ili kutimiza ahadi yake ya kujenga upya uchumi wa taifa, taasisi na miundombinu iliyoharibika. Na kuahidi kutengeneza barabara nyingi zaidi iwapo atachaguliwa tena.

Katika uchaguzi wake wa mwaka 2017, aliahidi kubuni nafasi za kazi na kuwekeza katika elimu, lakini wakosoaji wanasema ameshindwa kutimiza ahadi zake.

Alichaguliwa mwaka 2017 katika mabadiliko ya kwanza ya kidemokrasia nchini humo katika kipindi cha zaidi ya miaka 70, anagombea dhidi ya wagombea wengine wa urais 19, akiwemo kiongozi wa upinzani Joseph Boakai mwenye umri wa miaka 78, wa Chama cha Unity, kinachoonekana kuwa mpinzani wake mkuu.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Reuters na AFP

Forum

XS
SM
MD
LG