Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumatatu liliidhinisha operesheni ya usalama inayoongozwa na Kenya katika taifa la Caribbean, ambako uchumi umeporomoka na magenge yenye ghasia yanadhibiti eneo walilolinyakua kutoka kwa serikali dhaifu.
Viongozi wa nchi hiyo wanaokabiliwa na matatizo waliomba msaada wa kimataifa kwa mwaka mmoja ili kurejesha utulivu, lakini kumbukumbu ya hatua nyingine zilizoshindwa nchini Haiti zilizuia watu kujitolea.
Kisha Julai, muokozi alitokea: Kenya ilisema polisi wake 1,000 wanaweza kuongoza ujumbe huo, ofa hiyo ililifurahiwa na Marekani na wengine ambao walikataa kuwapeleka polisi wake wenyewe.
Kwa ruhusa ya Umoja wa Mataifa, Wakenya wametambua ukweli kwamba polisi wao katika siku za karibuni watakuwa wakipambana na majambazi wenye silaha nzito katika taifa geni na la mbali, na kuanza kuuliza maswali.
"Misheni yao ni nini huko Haiti?" aliuliza Emiliano Kipkorir Tonui, mwanajeshi wa zamani wa kulinda amani ambaye alisimamia Kenya ilipopeleka kikosi chake nchini Liberia, Timor Mashariki na Yugoslavia ya zamani, miongoni mwa nchi nyingine.
"Wakenya lazima wafahamishwe. Uongozi unawajibika kwa wananchi," Brigedia jenerali mstaafu aliliambia shirika la habari la AFP.
Wabunge Jumatano walitangaza kuwa watawaita mkuu wa polisi nchini Japhet Koome na Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki ili kupata ufafanuzi kuhusu ujumbe huo, ambao baadhi ya wataalam wa sheria wanapendekeza kuwa ni kinyume cha katiba.
Rais William Ruto alisema ni "misheni ya ubinadamu" katika taifa lililoharibiwa na ukoloni, huku Waziri wa Mambo ya Nje Alfred Mutua akisema Kenya inafanya "mapenzi ya Mungu" kwa kusaidia vizazi vya watumwa wa Kiafrika huko Haiti.
Forum