Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 22, 2024 Local time: 16:36

Mamlaka ya Mapato Kenya kuwatumia mawakala kupita kila nyumba kuhakikisha wanazingatia ulipaji ushuru


Maafisa wa Mamlaka ya Mapato pamoja na maafisa wa Huduma za Wanyamapori nchini Kenya wakiwa na meno ya tembo yaliyokamatwa katika bandari kuu ya Mombasa. Picha na STRINGER / AFP.
Maafisa wa Mamlaka ya Mapato pamoja na maafisa wa Huduma za Wanyamapori nchini Kenya wakiwa na meno ya tembo yaliyokamatwa katika bandari kuu ya Mombasa. Picha na STRINGER / AFP.

Mamlaka ya Mapato nchini Kenya, KRA, imeanza kuwatumia mawakala wake ambao wamefuzu mafunzo kubisha kwenye milango ya Wakenya na wafanyabiashara ili kuthibitisha wanazingatia ulipaji ushuru ili kuongeza mapato ya serikali.

Mawakala hao wapatao 1,400 ambao ni maafisa waliohitimu mafunzo katika Shule ya Mafunzo ya Kuajiri Wanajeshi huko Eldoret mwezi uliopita, mbali na kubisha hodi majumbani na madukani kuhakikisha ulipaji ushuru unazingatiwa ili kuongeza zaidi mapato ya serikali.

Pia maafisa hao watakuwa na wajibu wa kuwezesha usajili wa biashara mtandaoni, na kuwasaidia walipa ushuru kuthibitisha kodi anayotakiwa kulipa na kuweza kuwatambua wafanyabiashara wanaokwepa kodi.

Pia kuthibitisha maelezo ya walipa ushuru pamoja na kuhakikisha kanuni za mifumo ya ulipiaji kodi na ukusanyaji wa data za walipa ushuru zinasaidia mifumo ya ndani.

Raia wa Kenya watakuwa na uwezo wa kubofya alama ya nyota kisha nambari 572 halafu alama ya reli kwenye simu au kwenye wavuti wake kuthibitisha kuwa afisa aliyewasili kwake ni wakala wa mamlaka hiyo, ujumbe uliotumwa kwa walipa kodi mbalimbali unaeleza.

Utaratibu huu unatajwa kama sehemu ya mpango wa serikali ya rais William Ruto ya kuongeza mapato zaidi ya jumla ya shilingi trilioni 2.9 kugharamia bajeti yake ya shilingi trilioni 3.67 kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa fedha.

Serikali ya Kenya, kupitia Mkakati wa Mapato ya Muda wa Kati kwa Mwaka wa Fedha wa 2024/25 hadi FY 2026/27, imekiri kuwa ina pengo, kwa mujibu wa data za Benki ya Dunia na Shirika la Kimataifa la Fedha, IMF zinazoonyesha kuwa uzingatiaji ulipaji ushuru ni mojawapo ya njia zinazochangia kupunguza malimbikizo ya ushuru nchini Kenya.

Data hizo za Mwaka wa Fedha wa 2022/23, zinaonyesha kuwa pengo la ushuru nchini Kenya kwa sasa linakadiriwa kuwa asilimia 11.5 ya Pato la Taifa na kuna haja ya kuongeza wigo wa mapato.

Wafanyabiashara Kenya wakisubiri wateja katika soko la Marikiti huko Nairobi. Picha na SIMON MAINA / AFP.
Wafanyabiashara Kenya wakisubiri wateja katika soko la Marikiti huko Nairobi. Picha na SIMON MAINA / AFP.

Ili kufanikisha Mkakati wa Mapato ya Muda wa Kati kwa Mwaka wa Fedha wa 2024/25 hadi FY 2026/27, serikali kupitia wizara ya fedha, imependekeza kutekeleza hatua mbalimbali za usimamizi wa ushuru kuimarisha uzingatiaji wa walipaji kwa kutumia teknolojia kuboresha ufanisi, uwazi na huduma kwa wateja na kwa ufuatiliaji kwa wakati muafaka wa ulipaji huo.

KRA inalenga kukusanya shilingi trilioni 2.768 kufikia mwisho wa Mwaka wa Fedha wa 2023/2024 na kuzidisha kiwango hicho hadi shilingi trilioni tatu itakapofika Mwaka wa Fedha wa 2024/2025.

Pia, serikali inalenga kuunganisha mifumo yake ya usimamizi wa ushuru kuwezesha utoaji wa habari kamili kuhusu mapato, kuangalia uwezo wa mapato wa shughuli za kibiashara na kiasi kinacholipwa kama kodi kwa serikali.

Mamlaka hiyo mwaka 2021 ilikuwa imetangaza kuwa itachunguza mitindo ya maisha ya raia wa Kenya kwenye mitandao ya kijamii na majukwaa mengine ya kidijitali ili kubaini iwapo mapato yao yanalipiwa ushuru kulingana na mtindo wa maisha wanaonyesha, hasa kwa wale waliokuwa wakitundika picha zinazoonyesha magari ya kisasa na nyumba za kifahari lakini wanakwepa kulipa ushuru.

Mamlaka hiyo kulingana na data zake, imedumisha mwelekeo wa juu katika ukusanyaji wa mapato, baada ya kurekodi ukuaji wa asilimia 6.7 katika mwaka wa kifedha wa 2022/2023. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, KRA imerekodi mapato yaliongezeka kutoka shilingi trilioni 1.58 mwaka 2018 hadi kufikia shilingi trilioni 2.166 katika Mwaka wa Fedha wa 2022/23 uliokamilika mweizi Juni, ambao ukuaji wa asilimia 37 sawa na shilingi bilioni 586.2.

IMEANDARIWA NA KENNEDY WANDERA, VOA, NAIROBI.

Forum

XS
SM
MD
LG