Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Novemba 22, 2024 Local time: 15:39

Kenya: Viongozi wa dini na vuguvugu linalopinga masuala ya jinsia moja wakosoa uamuzi wa mahakama


Sheikh Mohammed Khalifa akizungumza na wanahabari nchini Kenya. Picha kwa hisani ya CIPK.
Sheikh Mohammed Khalifa akizungumza na wanahabari nchini Kenya. Picha kwa hisani ya CIPK.

Viongozi wa dini ya Kiislamu na vuguvugu linalopinga masuala ya jinsia moja  Mombasa, wamekemea na kupinga uamuzi wa Mahakama ya Juu kuhusu uhuru wa haki ya jamii ya wapenzi wa jinsia moja kutangamana na kujiandikisha kama shirika lisilo la kiserikali.

Viongozi hao wanasema kuwa uamuzi huo unakiuka maadili ya jamii za Kiafrika na mafunzo ya dini.

Wakizungumza na vyombo vya habari Mombasa, viongozi hao wameelezea hofu kwamba uhuru wa jamii hiyo, huenda ukachangia vijana wengi kujihusisha na masuala hayo ambayo yanakiuka dini, maadili na tamaduni za Kiafrika.

Wakiongozwa na katibu mkuu wa baraza la maimamu na wahubiri Kenya, CIPK, Sheikh Muhammad Khalifa, amesema kwamba wao kama viongozi na Wakenya hawatambui uamuzi huo na kwamba ni sharti rais na bunge la Kenya kuingilia kati kutumia sheria kupinga uamuzi huo.

“Tunamuambia rais William Ruto yeye na naibu wake pamoja na wake zao, ni wakristo wanaokwenda kanisani, tafadhali hili ni jambo lakuharibu maadili ya nchi ya Kenya, na kuharibu heshima ya wananchi wa Kenya asilikubali na bunge pia lihakikishe hili jambo halitakuwa katika nchi ya Kenya,” Sheikh Muhammad Khalifa, katibu mkuu wa CIPK.

Vuguvugu linalopinga uhuru wa jamii ya LGBTQ , wamekariri kuwa japo wanaheshimu mahakama, kamwe hawako pamoja na uamuzi huo kwa sababu Katiba ya Kenya inapinga ndoa za watu wa jinsia moja .

Aidha wamemtaka raia William Ruto kufuata mfano wa taifa la Uganda katika vita dhidi ya watu wanaoendeleza mapenzi ya jinsia moja kwani Afrika iko na tamaduni zake ambazo hazilingani na masuala hayo.

Naibu mwenyekiti wa vuguvugu hilo, Athuman Sharrif, amesema kuwa kutolewa uhuru wa kuunda vyama na kutangamana kutatoa fursa kwa maswala mengi yanayokiuka maadili ya kijamii, kusambaa Kenya.

“Katika uamuzi wa kwanza majority ya Wakenya walikemea jambo hili, hadi rais na wabunge pia walikemea lakini uamuzi huo ni kama watu hawakukemea na hili ni tusi kwa wakenya. Kufungua mlango wa LGBTQ Kenya ni kufungua nafasi kwa machafu mengine, kuna watu wanaitwa zoophile wanapenda kufanya mapenzi na wanyama nao pia watakuja kuomba haki yao, kuna wengine wapenda kufanya mapenzi na watoto wadogo pia nao watakuja, hata wauzaji bangi na pombe pia watakuja omba haki zao. Tunapinga kabisa.” Athuman Sharrif , naibu mwenyekiti wa anti LGBTQ movement.

Kwa upande wake Farida Rashid mwanaharakati Mombasa, ameelezea hofu kwamba shule za humu nchini huenda zikafunza maswala hayo ambapo hali hio itakua hatari kwa kizazi cha kisasa na kijacho.

Wakitoa uamuzi huo Majaji Philomena Mwilu naibu Jaji Mkuu Kenya na Jaji Smokin Wanjala walisema kuwa kubagua jamii ya wapenzi wa jinsia moja kutangamana na kujiandikisha kama shirika lisilo la kiserikali ukiukaji wa katiba katika kipengee cha 27(4) ambacho kina zungumzia kwamba serikali haitabagua mtu katka uhuru wa kutangamana kwa sababu ya jinsia, dini, jamii kabila na mengineyo.

Naye Mbunge katika bunge la Taifa , Peter Kaluma , ameapa kupinga uamuzi wa mahakama hio kwa kutuma ombi la kutaka kipengee hicho cha katiba nambari 27(4) kufanyiwa marekebisho kwa kufafanua jinsia kwa kujumuisha mwelekeo wa kijinsia.

“Hii itaziba mianya ya kikatiba ambayo mahakama inatumia kuanzisha ushoga na usagaji nchini kwa kile kinachodaiwa kuwa tafsiri ya mahakama. Na kulinda kwamba maswala ya utungaji sheria ni jukumu la bunge na nguvu ya kutengeza katiba inasalia na raia.” Peter Kaluma, mbunge homabay Town , Kenya.

Kesi hii ya LBTQ kutaka haki ya kujisajili ilijiri miaka 10 iliopita wakati bodi ya usajili wa mashirika yasio ya serikali ilipokataa kusajili jamii hio kama shirika lisilo la serikali, wakisema kuwa ingekuza tabia hizo za wapenzi wa jinsia moja kenya.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Amina Chombo, Kenya.

Forum

XS
SM
MD
LG