Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 22, 2024 Local time: 21:25

Azimio la Nairobi kuwa msingi wa mkutano wa hali ya hewa wa Dubai


Rais wa Ethiopia Sahle-Work Zewde (katikati) akipungia mkono akiwa na mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki (kulia) na viongozi wengine wa Afrika huko Nairobi, Septemba 6, 2023. Picha na Luis Tato / AFP.
Rais wa Ethiopia Sahle-Work Zewde (katikati) akipungia mkono akiwa na mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki (kulia) na viongozi wengine wa Afrika huko Nairobi, Septemba 6, 2023. Picha na Luis Tato / AFP.

Wajumbe wa mkutano wa hali ya hewa uliofanyika nchini Kenya umeidhinisha Azimio la Nairobi ikiwa ni mkakati wa pamoja na msimamo wa Afrika kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na litakuwa ni msingi wa mazungumzo yao katika mkutano wa COP28 utakaofanyika Dubai mwezi Novemba.

Marais wasiopungua kumi na watano kutoka nchi mbalimbali barani Afrika, walihudhuria na watunga sera, viongozi wa serikali, watoa maamuzi, wanasayansi, mashirika ya kimataifa na mashirika ya kiraia, na sekta binafsi

Lengo kuwa ni kufanikisha nguvu za pamoja za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na kutoa ufadhili unaohitajika kuimarisha nguvu za kijamii kuzikabili athari za mabadiliko hayo, na mishtuko mingine.

Viongozi wa Afrika, wadau mbalimbali, zikiwemo serikali, sekta binafsi, benki za kimataifa na wahisani, wametoa ahadi ya kuchangia jumla ya dola bilioni 23 za Kimarekani kufadhili ukuaji wa kijani, kupunguza na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kote barani Afrika.

Katibu Mtendaji wa Umoja wa Mataifa wa Mkataba wa Mfumo wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa (UNFCCC) Simon Stiell akiwa na viongozi wengine huko Nairobi, Septemba 4 2023. Picha na REUTERS/John Muchucha
Katibu Mtendaji wa Umoja wa Mataifa wa Mkataba wa Mfumo wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa (UNFCCC) Simon Stiell akiwa na viongozi wengine huko Nairobi, Septemba 4 2023. Picha na REUTERS/John Muchucha

Wakionyesha nia ya dhati ya kujitolea katika mustakabali endelevu wa Afrika na mifumo ya nishati unaouwiana na Azimio la Nairobi, viongozi hao wametia saini mkataba wa Hidrojeni ya Kijani na Umoja wa Ulaya kuendeleza na kuharakisha utengenezaji wa kijani kama mfumo wa uzalishaji wa shughuli rafiki kwa mazingira ambapo wafanyakazi watatumia rasilimali chache za asili kupunguza uchafuzi wa mazingira na taka, wakati wakichakata na kutumia tena nyenzo, na uzalishaji wa wastani ili kubuni maelfu ya ajira mpya zenye thamani ya juu pamoja na kuvutia uwekezaji mkubwa wa binafsi barani Afrika.

Ushirikiano wa kuleta mabadiliko ya nishati umewezesha uwekezaji wa dola milioni 60 za Kimarekani nchini Burunidi kwa miaka miwili kupanua ufikiaji wa nishati kwenye gridi ya taifa kwa watu wanaoishi vijijini.

Mwenyeji wa mkutano huo, rais wa Kenya William Ruto, ametangaza kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umeahidi dola bilioni 4.5 za Kimarekani kuongeza nishati mbadala kote barani Afrika kuchochea uwezo wa Afrika wa nishati safi ili kukidhi ugavi na mahitaji yaliyopo na yanayoongezeka.

Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua walipowasili kwenye mkutano wa Kilele wa Hali ya Hewa barani Afrika (ACS) 2023 Septemba 5, 2023. Picha na REUTERS/ Monicah Mwangi
Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua walipowasili kwenye mkutano wa Kilele wa Hali ya Hewa barani Afrika (ACS) 2023 Septemba 5, 2023. Picha na REUTERS/ Monicah Mwangi

Wakati serikali ya Marekani tayari imetangaza kitita cha dola milioni 30 za ziada kuharakisha juhudi za uzalishaji wa chakula kwa mazao yanayostahimili mabadiliko ya hali ya hewa kote barani Afrika.

Pia bara la Afrika limepokea michango mikubwa kutoka mataifa ya Ulaya, na uwekezaji mkubwa kutoka mashirika ya sekta binafsi kama Masdar, PowerGen, Leapfrog, Cross Boundary na Husk Power, itakayowezesha nchi nyingi za Afrika katika mipango yake ya kuzalisha nishati safi.

Viongozi wa Afrika wameonyesha wasiwasi kuwa, licha ya Afrika kuwa na makadirio ya asilimia 40 ya rasilimali za nishati safi duniani, ni dola bilioni 60 tu au asilimia mbili ya uwekezaji wa nishati mbadala wa dola trilioni tatu katika muongo uliopita uliokuja barani Afrika.

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir Mayardit na rais wa Eritrea Isaias Afwerki walipowasili katika mkutano huo, Septemba 5 2023. Picha na REUTERS/John Muchucha
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir Mayardit na rais wa Eritrea Isaias Afwerki walipowasili katika mkutano huo, Septemba 5 2023. Picha na REUTERS/John Muchucha

Kufikia lengo la Giga Wati 300 (GW) ifikapo mwaka 2030 kwa gharama inayokadiriwa ya dola bilioni 600 kunatafsiriwa kuwa ongezeko la mara kumi la mtaji wa kifedha unaoingia katika sekta ya nishati safi ya Afrika katika miaka saba ijayo.

Wakuu wa nchi za Afrika, sasa wanatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za dharura kupunguza hewa chafu, kutimiza wajibu wake, kutimiza ahadi zilizopita, na kuunga mkono bara la Afrika katika kushughulikia mabadiliko ya hali ya hewa, hasa kwa utekelezaji wa malengo yaliyowekwa katika Mkataba wa Paris.

Aidha, Rais Ruto ameeleza kuwa msimamo wa Afrika ni kwamba kuna haja ya kuwapo mageuzi ya usanifu wa fedha wa kimataifa na uhamasishaji wa rasilimali fedha za kutosheleza maendeleo wakati wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

IMEANDIKWA NA KENNEDY WANDERA, SAUTI YA AMERIKA, NAIROBI.

Forum

XS
SM
MD
LG