Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 22, 2024 Local time: 17:30

Walemavu ni miongoni mwa makundi Tanzania yanayodaiwa kutoshirikishwa katika uongozi


Baadhi ya washiriki wakiwasilisha mada zao katika maadhimisho ya demokrasia yaliyoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD)
Baadhi ya washiriki wakiwasilisha mada zao katika maadhimisho ya demokrasia yaliyoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD)

Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimetoa ripoti iliyoonyesha mafanikio katika kuimarisha demokrasia nchini huku kukiwa na ushiriki mdogo wa vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu katika nafasi za uongozi.

Ripoti hiyo pia imesema vyama vingi vya siasa kunyimwa ruzuku ya serikali, ni miongoni mwa matatizo yanayoikabili demokrasia ya Tanzania.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, licha ya kuwepo kwa ongezeko la ushiriki wa wanawake katika siasa na vyombo vya maamuzi ya kisiasa, bado haijafikia viwango vya kitaifa na kimataifa huku sababu ikiwa ni sheria kutovilazimisha vyama vya siasa kuteua wagombea wanawake isipokuwa kupitia viti maalum.

Anna Kulaya mkurugenzi wa shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo barani Afrika (WILDAF) anasema ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika siasa sheria zinapaswa kuweka ulazima wa kuwashirikisha katika masuala ya siasa kuanzia kwenye sheria za vyama vya siasa na sheria za uchaguzi.

“Sheria iweke kanuni kwamba lazima kuwepo na asilimia fulani ya wanawake, wanawake wengi kwenye majimbo na wanawake wataingia kwenye majimbo iwapo tu tutapata marekebisho ya sheria za vyama vya siasa, mabadiliko ya katiba na sheria za uchaguzi” amesema Kulaya.

Takwimu zilizotolewa na Kituo cha Demokrasia Tanzania kupitia ripoti hiyo zinaonyesha idadi ya sasa ya wanawake katika Bunge ni 144, ambapo 26 pekee kati yao walichaguliwa moja kwa moja huku 113 wakichaguliwa kupitia viti maalumu wawili kutoka Zanzibar na Watatu wakichaguliwa na Rais ikionyesha idadi ndogo zaidi ya wanawake wanaochaguliwa moja kwa moja kutoka kwenye majimbo.

Esther Thomas Naibu Katibu Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo anasema changamoto kubwa inayopelekea wanawake wengi kutochaguliwa moja kwa moja kutoka majimboni ni ukosefu wa fedha za kuendeshea kampeni wakati wa uchaguzi.

“Ukitaka kwenda kugombea jimboni lazima uwe na pesa itakayokuwezesha kushinda hilo jimbo wito wangu ni kuwa tutengeneze mazingira ya kuwawezesha wanawake kuweza kujiimarisha kiuchumi ili waweze kushindana na wanaume kwenye majimbo” amesema Thomas.

Aidha changamoto nyingine iiliyotajwa katika ripoti hiyo ni vyama vya siasa kukabiliwa na uhaba mkubwa wa rasilimali kutokana na vyama hivyo kutegemea ruzuku kutoka serikalini kama chanzo kikuu cha fedha, huku ni vyama vichache tu ndiyo vinakidhi vigezo vya kupata ruzuku.

Ocheki Msuva mkurugenzi wa shirika la Bridge for Change linalojishughulisha na kuhamasisha ushiriki wa vijana na wanawake katika masuala ya demokrasia anasema serikali inapaswa kutoa ruzuku kwa vyama vyote hata ambavyo havijakidhi kigezo vya kuwa na uwakilishi bungeni.

Baadhi ya washiriki wakifuatilia maadhimisho hayo
Baadhi ya washiriki wakifuatilia maadhimisho hayo

Msuva ameongezea kuwa “asilimia kumi ya ruzuku wanayopata kutoka serikalini itumike kuvipa hivi vyama ambavyo havina uwakilishi Bungeni”.

Hata hivyo, ripoti inabainisha kuwa ushiriki wa vijana na watu wenye ulemavu katika demokrasia unaendelea kubaki kitendawili, licha ya jitihada mbalimbali za kukuza ushiriki wao katika siasa na uongozi.

Msuva anasema vijana wamekuwa wakitumiwa kama chombo cha kufanikisha malengo ya kisiasa ya wanasiasa wakubwa, mara nyingi wakihusishwa na kampeni za uchaguzi na maandamano, lakini hawapewi nafasi za uongozi.

“Kijana anaweza akagombea kwenye nafasi na akashinda lakini akaambiwa asubiri apewe kwanza mwenye umri mkubwa kwahiyo matawi ya vijana yamekuwa kama vyumba vya kuwasubirisha vijana kwenye uongozi” amesema Msuva.

Moja ya mapendekezo katika ripoti hiyo ni kuwa sheria zinapaswa kuweka viwango maalum vya uwakilishi kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika nafasi za uongozi wa vyama na uteuzi wa wagombea wa nafasi za uchaguzi.

Imeandaliwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika.

Forum

XS
SM
MD
LG