Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Novemba 08, 2024 Local time: 10:12

Marekani yaihimiza Tanzania kufanya uchunguzi wa mauwaji ya afisa wa upinzani


Ali Mohamed Kibao, Kada wa chama cha Chadema Tanzania
Ali Mohamed Kibao, Kada wa chama cha Chadema Tanzania

Marekani imetowa wito leo Jumatatu kwa serikali ya Tanzania kufanya uchunguzi kutokana na mauaji ya afisa wa upinzani, Ali Mohamed Kibao ambaye mwili wake ulipatikana mwishoni mwa wiki baada ya chama chake kusema alipigwa na kumwagiwa tindikali.

Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania siku ya Jumatatu Septemba 9, 2024, umetoa taarifa inayowahimiza maafisa wa Tanzania kufanya uchunguzi huru, wazi na wa haraka kuhusiana na mauaji hayo.

Mauaji ya Kibao, afisa wa chama cha upinzani cha Chadema, yametokea mwezi mmoja baada ya viongozi wengine wa chama hicho kukamatwa wakati wa msako uliozusha wasi wasi kuhusu kurudi tena ukandamizaji wa kisiasa nchini Tanzania.

Taarifa ya Ubalozi wa Marekani iliyochapishwa kwenye ukurasa wake wa X inaeleza kwamba mauaji na kutoweka kwa watu pamoja na kukamatwa mwezi uliopita na kupigwa watu pamoja na juhudi nyinginezo za kuwateka wananchi kabla ya uchaguzi, ni mambo yasiyokubalika katika demokrasia.

Maoni kama hayo yalitolewa na Rais Samia Suluhu Hassan siku ya Jumapili, alipotoa salaama zake za rambi rambi na kutaka polisi kufanya uchunguzi wa kina na haraka kuhusiana na kifo cha Kibao.

Tanzania inajitayarisha kwa uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi Novemba na uchaguzi mkuu baadaye mwakani.

Kwa upande mwingine akihudhuria mazishi ya Kibao mjini Tanga siku ya Jumatatu waziri wa mambo ya ndani Hamad Masauni alitoa rambi rambi na kusema hawawezi kuruhusu kitendo hicho kupita bila ya kuchunguzwa.

Lakini baadhi ya viongozi wa chama cha Chadema na wakazi wa mji wa Tanga walimtaka waziri Masauni kujiuzulu, huku wengine wakimtaka aondoke kwenye ibada ya maziko hayo.

Forum

XS
SM
MD
LG