Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 14:03

Wachambuzi wa siasa nchini Tanzania waomba wananchi washirikishwe katika masuala ya Demokrasia


Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Febrauari 4, 2024. Picha na Tchandrou Nitanga / AFP.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Febrauari 4, 2024. Picha na Tchandrou Nitanga / AFP.

Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Demokrasia, wachambuzi wa masuala ya siasa nchini Tanzania wameeleza kuwa ushiriki mdogo wa wananchi katika masuala ya demokrasia unadhoofisha maendeleo ya kisiasa na kupunguza uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi pamoja na kukwamisha maendeleo ya taifa.

Wemetoa wito kwa serikali na wadau mbalimbali kuuelimisha umma juu ya umuhimu wa kushiriki katika utawala ili kuimarisha misingi ya demokrasia.

Wachambuzi hao wamesema ili kupatikana kwa Demokrasia ya kweli kunahitaji kuwepo kwa ushiriki mkubwa wa wananchi katika utawala pamoja na wananchi kufuatilia uwajibikaji wa viongozi wao na kuwa na uwezo wa kuwawajibisha viongozi wanapokosea.

Buberwa Kaiza Mchambuzi wa masuala ya Siasa kutoka Dar es Salaam amesema kutokana na uchache wa uelewa wa wananchi juu ya masuala ya Kidemokrasia wananchi wamekuwa hawashiriki moja kwa moja kwenye masuala ya utawala na hivyo kupelekea viongozi kutosikiliza maoni ya wananchi.

“Bado wananchi wanasikiliza zaidi viongozi kuliko viongozi kusikiliza wananchi na huu umekuwa utamaduni wa Tanzania ambao bado wananchi hawajioni kama wao ndio mamlaka ya nchi na viongozi ni watumishi wao wananchi waliowengi kutokana na kutokuwa na taarifa sahihi juu ya masuala ya utawala na demokrasia wanajiona kwamba wao ni watumishi wa viongozi na viongozi wanafikiri hivyo na wenyewe.”

Wachambuzi wanaongezea kuwa kushindwa kushiriki kikamilifu kwa wananchi katika masuala ya kidemokrasia kunapelekea changamoto mbalimbali ikiwemo kupungua kwa uwajibikaji wa viongozi, kukokesekana kwa haki za kiraia, pamoja na kuhatarisha misingi muhimu ya kidemokrasia suala ambalo linaathiri maendeleo ya jamii na uchumi wa Taifa.

Prof Xavery Lwaitama Mwandamizi mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema ili kuleta uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi wao, Viongozi wote wanaotoa maamuzi katika jamii wanapaswa kuchaguliwa kutoka katika jamii hiyo ili kuwapa raia haki ya kuwahoji viongozi hao kuliko baadhi ya viongozi kuteuliwa na Rais wa nchi.

“ Hata hawa viongozi kama Mtendaji wa Kata, Mtendaji wa tarafa, Mkuu wa wilaya, Mkuu wa Mkoa wachaguliwe watokane na watu wa kwenye jamii hiyo ndio kujitawala kwamba viongozi wote wanaotoa maamuzi wote watokane na kuchaguliwa kutokana na wale ambao wanatoa maamuzi juu yao yaani mtu anaetoa maamuzi juu yako akiwa anatokana na nyie na mnaweza mkamuondoa saa yoyote mnapoona hawatekelezei mambo yenu hapo mnasema sasa mmepanua demokrasia.”

Hata hivyo Mwandishi wa habari Mkongwe Jenerali Ulimwengu kutoka Dar es Salaam amesema ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika masuala ya kidemokrasia ni muhimu kwa jamii kuelimishwa ili waweze kuelewa nafasi yao katika demokrasia na umuhimu waushiriki wao.

“Watu walio na uelewa mkubwa zaidi waliofumbuka macho mapema zaidi waendelee kuwaelimisha na kuwaamsha na kuwahamasisha hao waliowengi ambao hawaelewi juu ya demokrasia hao watakuwa ni walimu kwa wale ambao bado wanadhani kujengewa mabwawa na mabarabara ndio mwisho wa hadithi.”

Kaiza amemalizia kwa kuhimiza vyama vya siasa nchini kutimiza wajibu wao wa kukuza demokrasia na amevitaka vyama vya upinzani kuandaa sera zenye manufaa kwa wananchi badala ya kutumia muda mwingi kugombana na chama tawala, hali inayosababisha kusahau majukumu yao ya msingi katika kuimarisha demokrasia.

Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam.

Forum

XS
SM
MD
LG