Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 10:11

Wafanyakazi wa JKIA wapambana na maafisa wa usalama Kenya


Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Nairobi, April 28, 2016.
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Nairobi, April 28, 2016.

Wafanyakazi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi nchini Kenya, wamesitisha mgomo wao baada ya siku nzima ya makabiliano na maafisa wa usalama waliokuwa wanazuia maandamano.

Mgomo unahusu kandarasi za wafanyakazi na usalama wa kazi zao kufuatia juhudi za kuunda mkataba kati ya shirika la ndege la Kenya Airways na muungano wa wafanyakazi wa safari za ndege, shirika hilo likipangiwa kusimamia shughuli za uwanja wa JKIA.

Kwa nini Kenya Airways?

Kiongozi wa muungano wa wafanyakazi waliyogoma Moss Ndiema amekamatwa muda mfupi kabla ya wafanyakazi kuahirisha mgomo.

Benjamin Okwach, ambaye ni mmoja wa wafanyakazi waliokuwa wakiandamana, amesema haya: “Huwezi kuruhusu kampuni kama Kenya Airways, ambayo inaporomoka kibiashara, kusimamia Mamlaka ya Ndege Kenya. Mamlaka ya Ndege nchini Kenya inatengeneza takriban shilingi bilioni 11 za Kenya sawa na dola milioni 110 kwa mwaka.

"Shirika la ndege la Kenya limekuwa likipoteza shilingi bilioni 7, vipi shirika kama hilo liweze kupewa dhamana ya kusimamia mamlaka nyengine ambayo tayari inapata hasara ya shilingi bilioni 10 hadi 11 kwa mwaka. Hilo haliwezekani na hiyo ndio sababu tunapinga hilo. Kuna watu wachache, hasa wale waliokuwa ndani ya serikali, ambao wanataka kuuchukuwa uwanja wa ndege na hatuwezi kuacha hilo litokee."

Jibu la waziri wa uchukuzi

Lakini akijibu hoja hizo waziri wa uchukuzi James Macharia ametaja mgomo huo kuwa haramu, uhalifu wa kiuchumi na uhalifu mkubwa.

Macharia amesema : “Haustahili kutatiza vyombo vya usalama vilivyopo hasa iwapo huna msingi wa malalamishi yako, wakati una kazi. Hakuna mtu amekosa kukulipa, hakuna aliyetishia kazi yako, halafu unagoma. Umepewa hakikisho kwamba idadi ya ajira itaongezeka, nab ado unagoma. Huu ni uovu, uhalifu wa kiuchumi na ni jambo hatuwezi kuvumilia. Ni jambo la kihalifu ndio maanda maafisa wa usalama hapa ambao wamefukuza kila aliyekuwa analeta matatizo”.

Athari za mgomo huu

Mgomo huo umeathiri shughuli za usafiri, ndege zikibadilisha safari na kulazimika kutua Kisumu au Mombasa, huku safari za ndege 24 kutoka Jomo Kenyatta zikiahirishwa na kuathiri safari za mamia ya wasafiri.

Abiria Kingsley Akujimba –msafiri wa Kenya Airways ameeleza haya : “Tumepoteza pesa nyingi kwa sababu tumekosa ndege zinazopaa ndani ya nchi. Unapokosa ndege, unasahau pesa uliyokuwa unafuatilia. Ni vibaya sana, ni hasara kubwa”.

Wakati huohuo wafanyakazi wameendelea kugoma licha ya kuwepo amri ya mahakama kuzuia mgomo huo.

Shirika la ndege la Kenya airways linakabiliwa na hali ngumu ya kifedha na maafisa wanajaribi kutafuta mbinu za kuliondoa kutoka katika hasara kwa kulipokeza usimamizi wa uwanja wa ndege wa JKIA.

Imetayarishwa na wandishi wetu, Kennes Bwire, Washington, DC na Hubba Abdi, Nairobi, Kenya

XS
SM
MD
LG